Moyo wa Mchungaji, Itikio la Kanisa
Baba yake alikuwa wa imani ya Kibaha’i na alifanya uuguzi. Alidai kuponya watu na kumtayarisha mtoto wake kufuata nyayo zake. Kwa bahati mbaya, hakuweza kujiokoa kutokana na ugonjwa uliomwua.
“Baada ya baba yangu kufa, niliona uwezo wa juu zaidi kuliko ule wa baba yangu. Nilitamani kumjua Mungu, na mwaka wa 1998 nilitoa maisha yangu kwa Yesu na kubatizwa.” Leo mwana huyo ni Mchungaji Rurangwa Muziga Meshack, ambaye anatumikia pamoja na waumini wake na wachungaji wenzake kupeleka Injili kwa kuvuka mipaka.
Mchungaji Meshack ni kiongozi wa umisheni katika Kanisa la Good Shepherd Church Nairobi, Kenya. Kanisa hilo ni sehemu ya madhehebu ya Kanisa la Africa Gospel Church linalofuata mizizi yake ya mwaka 1932 kazi iliyofanywa na wamishenari kutoka World Gospel Mission. Lilianza likiwa kikundi cha kujifunza Biblia, na baadaye likawa kanisa la kufikia jamii ya jirani. Mnufaika wa kanisa mwenyewe, Mchungaji Meshack alikuwa akihusika kama mhudumu anayepata mafunzo kazini (mazoezi) alipofika Kenya kama mkimbizi kutoka DR Congo. Hatimaye, alipewa leseni ya kuwa mhudumu wa wakati wote na akateuliwa kuwa mchungaji wa umisheni.
Kila kitu huinuka na kuanguka kwa kutegemea uongozi
Umisheni ni shughuli kuu ya Kanisa la Good Shepherd Church. Kutoka makao yao makuu nchini Kenya, wameanzisha makanisa nchini Rwanda, Burundi, na mashariki mwa DR Congo. Kanisa lao linalofuata kuanzishwa liko Sudan Kusini. Kila kundi katika kanisa linahusika katika nyanja mbalimbali za umisheni—kuomba, kutoa kifedha, mafunzo, na kushiriki katika safari za kimishenari za ndani na za kimataifa.
“Kama John Maxwell alivyosema, ‘mambo yote huinuka na kuanguka kwa kutegemea uongozi’”, Mchungaji Meshack anatushirikisha. “Mchungaji hushawishi kanisa kwa ajili ya umisheni kupitia uongozi wa mfano. Kama mchungaji, ninahubiri na kuwafunza kusanyiko kuwa waaminifu kutii Agizo Kuu. Pia ninahusika katika kwenda na kutoa. Umisheni hauwezi kufanywa na mchungaji peke yake; washirika lazima pia waombe, watoe, na waitie moyo timu ya wachungaji.”
Hakuna kinachofanyika nje ya mpango wa kanisa, na lengo la utume la Good Shepherd limekita mizizi katika mikakati yao muhimu: kuinjilisha ambao hawajaokoka, kuanzisha makanisa, kuwajenga waumini, kuandaa viongozi, na kuonesha huruma. “Umisheni sio tu idara ya kanisa au shughuli; ndiyo sababu ya kanisa kuwepo, kwa hiyo tumejitoa kufanya hivyo,” Mchungaji Meshack anasema.
Maombi na mafunzo
Kila kitu huanza na maombi. Kanisa hukutana kila Ijumaa ya mwisho wa mwezi ili kuombea kila wanachofanya, ikiwa ni pamoja na umisheni. Timu yao ya maombezi pia hukutana Jumamosi kwa kusudi hilo. Wanaomba msaada wa Mungu kumtambua mtu anayefaa kumtuma kwenye umisheni, na kuwaonyesha ni nchi gani au eneo gani la kwenda. Wanachangisha pesa kwa maombi, wakimwomba Mungu awatume watoaji na kuwafanya watu wawe tayari kuunga mkono.
Mungu anapokuita katika huduma, Yeye huenda pamoja nawe na kukusaidia.
Kila mwaka, Oktoba ni mwezi maalum wa umisheni. Kanisa huwaalika watu kuzungumza juu ya mada maalum kuhusu umisheni na kuwahimiza washirika kutoa kwa ajili ya wamishenari na kwenda umisheni. Wanawafunza washirika kuwa na mtazamo wa Agizo kuu na kushirikisha Injili kwa njia ya urafiki, kutoa kwa wale wanaohitaji, na kuwaombea wanaoteseka.
Mchungaji Meshack anatushirikisha hadithi ya John: “Wakati kanisa lilipofanya mafunzo kuhusu kufanya wanafunzi kwa ufanisi, John alihudhuria na baadaye akapata nafasi ya mafunzo katika benki. Alianzisha wazo la kujifunza Biblia na vipindi vya maombi kila siku kabla ya kazi. Alipewa ruhusa, na kila mtu akapenda kujiunga. Wenzake wengi waliorudi nyuma walianza tena kusoma Biblia zao na kuhudhuria kanisa. Leo, wamepata chumba cha kukutana kwa ajili ya sala, ibada, na kujifunza Biblia. John alikuwa amechochewa na kile ambacho kanisa lilikuwa likifanya. Lengo letu ni kuwasaidia washirika wa kanisa kufuata hatua za Yesu kwa kuwafundisha kufanya wanafunzi.”
Uhamasishaji na uandaaji
Kanisa huwaandaa washirika walio tayari kuitikia wito wa Mungu Wanawafundisha kuhusu utamaduni wa watu, kanuni za mavazi na imani zao, na jinsi ya kuwasiliana. Kanisa hupanga safari za umisheni za muda mfupi na mrefu ndani na nje ya nchi, na washirika hujiandikisha kwenda wenyewe au kusaidia wale ambao wanataka kwenda lakini hawana pesa. Safari za kimataifa hufanywa kila robo mwaka au kulingana na mpango wao wa kanisa kwa mwaka. Wana bajeti ya kila mwaka ya umisheni na pia kutenga sehemu ya matoleo yao ya kawaida kwa madhumuni hayo. Kanisa lina maeneo matatu ya umisheni na wamishenari ambao wanawasaidia kifedha na kwa kuwatembelea mara kwa mara.
Hamasa ya Mchungaji
Kwa kusanyiko la watu 600 hivi, kufanya umisheni si rahisi. “Changamoto kubwa imekuwa fedha. Tunaendesha huduma zetu zote bila kutegemea msaada kutoka nje. Ubaya mwingine ni kwamba kusanyiko kwa sehemu kubwa ni la wahamiaji ambao huendelea kuhama. Ni vigumu kuwa na wafanyakazi wa kujitolea wa kudumu na washirika ambao wanaweza kushiriki kikamilifu katika kazi ya kanisa. Vikwazo hivi hutufanya tushindwe kutuma wamishenari zaidi, ingawa tungependa kufanya hivyo.”
Hata hivyo, anatoa ushauri na kutia moyo: “Mungu anapokuita katika huduma, Yeye huenda pamoja nawe na kukusaidia. Hii imeniongoza kumwamini Mungu, lakini yeyote anayetaka kuitikia wito wa umisheni wa Mungu lazima awe tayari kwa shida na furaha. Mtu hata hivyo hapaswi kuogopa au kutilia shaka mambo yanapokuwa magumu—hiyo ni sehemu ya wito wetu katika umisheni. Nimejifunza kutumia rasilimali zilizopo kufanya kile ninachoweza kwa wakati huo, badala ya kutofanya chochote. Huduma yetu inafanya kazi kwa imani; si kwamba tunaweza kujikimu, bali Mungu hutupatia mahitaji yetu kwa njia yake mwenyewe.
“Ili kanisa lijihusishe sana na umisheni, ni lazima lianzie kutoka moyoni mwa mchungaji. Wakati fulani kanisa linaweza kuhusika katika mambo mengi na kupoteza moyo wa umisheni. Mchungaji anapojua sababu ya kuwepo kwa Kanisa, umisheni kipaumbele chake.”