Jinsi Kanisa Letu Dogo Lilivyokuza Moyo Mkuu Wa Umisheni
By Mch.Moses Paye
Kama wachungaji, kwa kiasi kikubwa, tunaweza kusaidia kuonyesha mwelekeo wa makanisa yetu. Sehemu kubwa ya jukumu letu ni kutumia ushawishi wa kiroho kwenye maisha na mwelekeo wa watu walioko chini ya uangalizi wetu. Na ndiyo maana tunaitwa viongozi.
Kanisa letu la Evangelical Christian Fellowship (ECF) yaani ‘Ushirika wa Kiinjili wa Kikristo’ lililoko nje ya Jiji la Monrovia, nchini Liberia, tarehe 26 Juni 2016 lilifanya sherehe ya kuiaga familia ya wamishenari ambayo ilikuwa inaenda kufanya kazi ya Mungu katika maeneo ya vijijini nchini Liberia. Tunamtuma ndugu Dexter Brown na familia yake kwenda kwenye mkoa wa Kusini Mashariki ili kuinjilisha na kupanda makanisa. Ndugu Dexter alieneza kazi ya uinjilisti hadi vijiji vilivyoko katika sehemu za Sinoe na maeneo mengine yaliyo ndani zaidi.
Huu ni wakati wa kusisimua sana kwa familia ya kanisa letu, na tunamsifu Bwana kwa upendeleo na uongozi wa Roho kutuongoza hata kufika nje ya mipaka na mazingira ya kanisa letu na kuwashirikisha wengine habari za Injili.
Kanisa la ECF limekuwa likiisaidia familia ya Brown katika kutafuta msaada wa kipesa. Lakini zaidi sana kuwatia moyo wakristo wetu ili waweze kukubali na kushiriki kikanilifu katika kazi za umisheni.
Kuufanya Umisheni Uangaze na Kuonekana kwa Watu
Haya yamekuwa ni maombi yangu tangu kuanzishwa kwa kanisa kwamba umisheni ungekuwa ndio kusudio kuu la ECF. Katika mikutano yetu tumekuwa tunamwomba Bwana atusaidie ili tuwe watu wanaojali umisheni. Kila mwaka huwa tunautenga mwezi wa Tano kwa ajili ya umisheni. Umisheni ni kitovu cha mahubiri, mafundisho, nyimbo za kuabudu na maombi yetu. Tunasisitiza wajibu, kipaumbele, uzuri na thawabu kwa ajili ya kufanya umisheni, ambayo itawafanya watu wetu kutiwa moyo na kuchukua hatua za kushiriki katika kazi za umisheni. Huwa tunatoa matoleo maalum kila juma la mwezi wa Mei, ambayo kwa kawaida sadaka hiyo hupelekwa kwenye Bodi ya Umisheni ya kanisa la Kiinjili la Liberia (Evangelical Church of Liberia – ECOL), ili kusaidia kazi zake za kihuduma.
Mwaka 2009 nilianza mpango wa mwaka mmoja wa kufundisha Biblia ili kuwaandaa viongozi kwa ajili ya kutoa huduma ya umisheni. Karibu watu wote waliopata hayo mafunzo sasa wanatumika katika kanisa kwa uaminifu. Baada ya Dexter Brown kumaliza mafunzo 2010-2011, alitumika kama shemasi na mwalimu wa Shule ya Jumapili ya watu wazima.
Kwa miaka kadhaa hapo nyuma, mimi na mke wangu tuliongoza safari za kwenda kuhubiri vijijni. Kwa kawaida tuliwatia moyo washirika wa kanisa katika kuambatana nasi. Wengine waliungana nasi kwa ajili ya kuwashuhudia wanakijiji habari za Kristo. Waliporudi nyumbani, waliwaambia washirika wengine habari za kusisimua kuhusu kazi na mahitaji. Huduma hii ilisababisha kuanzishwa kwa makanisa matatu katika vijiji vitatu. Dexter mara nyingi aliambatana nasi safarini, na nilimwona akikuza hamasa kwa ajili ya roho za watu pale alipokuwa anawaambia habari za Yesu. Uamuzi wake wa kwenda kwenye uwanja wa umisheni haukuwa wa ghafla kama ajali; bali Bwana alikuwa amemwandaa.
Sababu ya kusherehekea
Kanisa la ECF lililopo Monrovia, lilianzishwa mwaka 2001, wakati vita ilipokuwa inaendelea nchini Liberia. Leo lina waumini 165, na tuna watu wanne ambao ni wahanga wa ugonjwa wa Ebola, wakiwemo yatima wawili.
Familia nyingi za kanisa, ikiwamo na familia ya Brown, waliwekwa chini ya karantini wakati ugonjwa wa Ebola ulipozuka. Mwanzoni mwa 2015, wakati ECOL ilipopiga mbiu kwa Makanisa mengine kutuma wamishenari kwenye mkoa wa Kusini Mashariki, tulikuwa mara kwa mara tukimwomba Mungu ili aguse mtu wa kwenda.
Miezi mitatu baadaye Dexter aliniambia, “Mchungaji, nina uhakika kuwa Bwana anataka mimi niende.” Dexter alisikia wito wa umisheni tangu alipomaliza mafunzo ya Biblia.
Yeye na familia yake wamekuwa wakiomba kwa ajili ya uongozi wa Mungu, kwa hiyo wito kutoka ECOL ulikuwa ni uthibitisho na jibu. Kama mchungaji wa ECF, namtukuza Mungu kwa kubadilisha kanisa letu kuwa mwili wa “waendaji” na “waunga mkono”! Inatupa furaha isiyo na kifani kuona waumini kusaidia huduma za umisheni. Ni jambo ambalo kila kanisa linapaswa kulifurahia na kulifanya.
Picha na Warwick Walker