Skip to content

Akina Mama wa Msaada Kusimama kwenye Pengo kwa Ajili ya Watoto wa Wamishenari

Furaha Kengela

Mnamo Februari 1996, bweni la watoto la EMS lilifunguliwa huko Jos, Nigeria, ili kuwapatia makazi watoto wa wamishenari wa EMS ambao walikuwa wakihudumu katika maeneo ya umisheni. Wazo hilo lilichochewa na kugundua kwamba asilimia 25 ya wamishenari waliacha umishenari kwa sababu ya ukosefu wa elimu bora kwa watoto wao. Kufikia mwaka uliofuata, bweni hilo lilikuwa limejaa, likiwa makazi kwa watoto 50. Matukio katika maadhimisho ya mwaka wa kwanza yalichochea kuzaliwa kwa shirika la kusaidia watoto la Akina Mama la EMS (EMS Children Support Mothers), ambalo baadaye likaitwa Support Mothers International (SMI).

Maadhimisho hayo yalifanyika katika viwanja vya shule ya wafanyakazi wa ECWA na kuleta pamoja watu wazima na watoto kutoka familia za SIM na EMS, waumini wa kanisa la ECWA, marafiki na watu wengine wenye kutakia wenzao mema. Kwa sababu bweni halikuwa na nafasi ya kuwahifadhi watoto wa wamishenari zaidi, tukio hilo lililenga kupata fedha kwa ajili ya upanuzi. Wake na watoto wa wamishenari wa SIM waliotoka ugenini walijitolea kuandaa viburudisho, na waliwahudumia wageni vizuri sana kiasi kwamba waliwagusa sana wanawake wa Nigeria waliohudhuria.

Kuzaliwa

Dkt. Lami Bakari Ibrahim, mwanzilishi wa SMI, anakumbuka kwamba baada ya tukio hilo, baadhi ya wanawake wa Nigeria walibaki nyuma na kuulizana, “Kwa nini baada ya miaka 100 ya kuwa na wamishonari wa SIM katika nchi yetu, bado wanatutumikia? Vipi kuhusu sisi wanawake wa kitaifa? Tunaweza kufanya nini?” Uchunguzi wao ulisababisha mkutano wa ufuatiliaji ambapo walikaribisha changamoto ya kukusanya fedha ili kupanua uwezo wa bweni. Walizungumza na marafiki na watu wao wa karibu, na kukusanya pesa za kutosha kujenga jengo imara. Huu ulikuwa mwanzo wa Akina Mama wa Msaada kusimama katika pengo la wazazi kwa ajili ya watoto wa wamishenari. Walitoa chakula, nguo, vifaa vya kusafishia, na kadhalika. Baadhi ya Akina Mama waliwakaribisha nyumbani kwao watoto wakati wa (likizo) mapumziko ya shule na wengine walitembelea bwenini mara mbili kwa wiki kwa ajili ya kujumuika na kufanya shughuli pamoja nao. Kwa pamoja, walitengeneza vitu vya ufundi kama vile kuunda upya kadi za Krismasi za zamani na kupamba viatu au kanda mbili kwa shanga.

Kukua

Akina Mama hawa walisafiri kote nchini ili kuleta ufahamu kwa watu kuhusu mahitaji ya watoto wa wamishenari wa EMS. Walichukua bidhaa za kutengeneza kwa mikono, ambazo sasa zina lebo, ‘Mwana-Kondoo wa EMS,’ na kuziuza ili kupata pesa wakati wowote walipopata nafasi ya kushirikisha mbele ya vikundi vya wanawake katika makanisa mengine. Baadhi ya watoto wa EMS walienda na kushiriki matukio hayo wakati Wamama hawa walipowashirikisha.

Dkt. Lami anaeleza kuwa akina mama hawapokei michango moja kwa moja. Wanashirikisha maono, na kutangaza mahitaji mbalimbali. Wanahimiza vikundi vya wanawake kutembelea bwenini na kujionea wenyewe maeneo yenye uhitaji wanayoweza kusaidia.

Matunda

Dkt. Lami anaeleza kwamba ingawa kikundi hiki kwa sasa hakijachangamka kama hapo awali, malengo yote ya awali ya kukianzisha yalitimia. Sio tu kwamba walipanua bweni; pia walinunua ekari tisa za ardhi, wakaweka majengo ya shule na ya wafanyakazi, na kuanzisha shamba la mifugo. “Tuliona tulichofanya kama kuhudumu katika umisheni, ingawa hatukuwa shambani kama wazazi wao,” Dkt. Lami anakumbuka. Kazi ya Akina Mama wa Msaada inaonyesha kwamba wakati wamishenari wanapohudumu kwenye mstari wa mbele, tukiwa kama familia ya kweli katika Kristo, sisi tulio nyumbani tunaweza kusimama katika pengo kwa njia za maana sana.