Wajibu wa mchungaji kuamsha moyo wa umisheni katika kanisa la Tanzania
Mwinj. Joel Nkanda Simbitti
Mimi nilizaliwa na kumwamini Yesu kwenye moja ya makanisa ya Kiinjili Tanzania (evangelicals). Chakushangaza ni kwamba nilijua kuwa umisheni ni kazi ya mzungu (white man’s work)! Nilipojiunga na chuo cha theologia, Scott Christian University, mwaka 1994 nilifumbuliwa macho. Mwalimu wangu, Dkt. Richard Gehman, alianza kukaribisha wamishenari wazalendo kwenye ibada za wanafunzi (chapel) kuja kutoa shuhuda zao. Nilishtuka sana wamisionari Wakenya wakitambulishwa kwenye ibada zetu! Mimi nilitarajia sana kumwona mmisionari kutoka nchi za Magharibi kama nilivyozoea kuwaona Tanzania. Hata hivyo shuhuda za wamisionari hao ziliugusa sana moyo wangu mpaka nilianza kulia machozi. Moyoni nilijisikia deni kubwa kwa ajili ya makabila mengi bila Injili ya Kristo Tanzania!
Matokeo yake niliyatoa maisha yangu kwa ajili ya umisheni na kupanda makanisa. Nilifundisha na kuhamasisha watu binafsi, makanisa, vikundi makanisani na vyuo vya Biblia/Theologia kufanya umisheni. Kwa uzoefu huo nikaelewa wajibu wa mchungaji kulifanya kanisa kuwa la kimisheni. Kwa mfano mwaka 2000 nilipeleka wanafunzi 2 kutoka chuo cha Biblia kwenda mafunzo kazini kwa Warangi mkoani Dodoma. Wanafunzi hao walifanya kazi na mmisionari mzalendo Peter Pharles Kisenna. Miaka 20 baada ya umisheni, Kisenna alianza kuchunga kanisa na alilolihamasisha kufanya umisheni. Baada ya kuongoza kanisa, Kisenna alikwenda kufundisha vyuo vya Biblia, na akiwa huko aliunda huduma ijulikanayo kama Triple Mission for Christ (TMC). TMC iliwaunganisha wanafunzi wa vyuo na wakristo makanisani kuunda timu ya kuyafikia makabila yasiyofikiwa. Mwaka 2022 Kisenna alichaguliwa kuwa Askofu kwenye dhehebu lake, kwa nafasi yake anawaongoza Wakristo kwenda kuwafikia Wataturu, Warangi na Wamasai katika mikoa mbalimbali nchini Tanzania.
Pia nimejifunza wajibu wa mchungaji katika huduma ya umisheni kupitia kuyahamasisha makundi ya kwaya za kufanya umisheni. Mwaka wa 2020 niliitwa na kwaya ya Vijana Geita kuwafundisha jinsi ya kufanya umisheni. Mwanzoni, mchungaji wao John Masanyiwa, hakuhamasika sana lakini baada ya kupokea maono, mchungaji huyo ndiye mbeba maono ya umisheni katika kanisa la Africa Inland Church Tanzania. Mpaka sasa Masanyiwa ameliongoza kanisa lake kuyafikia makabila ya Wanyambo, Wasonjo, Wamasai na Wabarabaig (Wamang’ati).
Mchungaji mwingine ni Samwel Lupilya aliyestaafu miaka 3 iliyopita. Lupilya alikuwa mmisionari kwa Wabarabaig kabla ya kwenda kuchunga makanisa. Hivyo alichunga makanisa ya Malya, Makongoro na Buzuruga na katika makanisa yote Lupilya aliwahamasisha Wakristo kuwafadhili, kuwasomesha na kuwategemeza wamisionari shambani. Kwa nia hiyo mchungaji huongoza timu kutoka makanisani kwenda kufanya umisheni na kupanda makanisa ndani na nje ya nchi. Kwa mfano ameongoza timu za kupanda makanisa kwa Wataturu licha ya safari za kimisheni kwenda Kongo (DRC) na Msumbiji.
Tukitaka kanisa la Kristo duniani liutii Utume Mkuu lazima wachungaji wabebe maono ya umisheni. Mchungaji akitaka kanisa lake liwe la kimisheni lazima afanye yafuatayo: (a) afundishe na kuhubiri umisheni (b) awakaribishe wamishenari kanisani (c) aliongoze kanisa lake kwenye safari za kimisheni (d) alipeleke kanisa kwenye safari za kimafunzo kwenye makanisa yanayofanya umisheni.
Mwinj. Joel N. Simbitti, Mkurugenzi wa Huduma za Kiroho AICT na Mratibu wa Mtandao wa Umisheni Tanzania.