Mchungaji wetu alifanya wito wetu wa kimishenari uwezekane
Patrick Nabwera
Maombi yamekuwa hitaji muhimu sana. Mke wangu na mimi hutumika mbali na nchi yetu, na mchungaji wetu huko nyumbani huhamasisha kusanyiko lote kutuombea. Angewaambia kwenye ibada ya Jumapili waangalie upande wa eneo letu la umisheni na kuomba, kisha anahitimisha maombi.
Wakati mmoja, mchungaji wetu hakuweza kutusaidia kifedha. Alinishika mkono na kuomba, “Mungu, hatuna cha kuwapa, lakini tunaomba kwamba uwafadhili.” Na kwa hakika, Bwana alitufadhili. Mchungaji wangu alikuwa mwaminifu, na nilijua hali hiyo. Wakati ulipofika, alihamasisha kanisa kutusaidia kwa rasilimali.
Wakati mwingine, alimtuma dada kututembelea katika eneo letu la umisheni, umbali wa kilomita 2500 kwa barabara. Kumuona dada huyu ilikua kama kumuona malaika. Uwepo wake haukuwa wa kutia moyo tu, bali pia fursa kwake ya kurudi na kumshirikisha mchungaji na kanisa uhalisia katika eneo letu la umisheni. Hii iliongeza maombi na hali yao kutujali.
Watoto wetu walikuwa katika shule si mbali na kanisa letu la nyumbani na mara nyingi, hatukuweza kuwatembelea kwa sababu ya umbali. Mchungaji wetu, mke wake, msaidizi wake, na baadhi ya washirika wa kanisa walikuwa wakiwatembelea. Msaada huu ulitufanya kujua hatuko peke yetu.
Wakati wa mapumziko yetu nyumbani, mchungaji wetu alitualika kushirikisha shuhuda zetu na kusanyiko. Baadaye, alijiunga na kikundi kidogo kilichokuja kusikiliza hadithi zaidi. Uwepo wake katika mkutano ulifanya wengine waone umuhimu wake. Kando na hili, kila mara alitengeneza muda wa kushirikiana, kusikiliza safari yetu ya umishenari, na hatua zinazofuata. Aliwakumbusha daima kusanyiko kututegemeza, na hilo likaongeza thamani ya kazi yetu machoni pa kanisa letu.
Ninalinganisha umisheni wa kwenda tamaduni tofauti na kutembea kwa miguu miwili. Mguu mmoja ni “unaenda” na mwingine “unatuma.” Kama vile inavyochosha, ni wa polepole na inachosha kuruka kwa mguu mmoja, ndivyo ilivyo kwa kufanya umisheni kwa mguu mmoja – kwenda bila kutuma. Paulo anauliza, “Na watawezaje kuhubiri isipokuwa wametumwa?” (Rum. 10:15a) Na Yohana anasema wale wanaotuma wanapaswa kutuma kwa namna impasayo Mungu (3 Yoh. 6).Na ufunguo wa kanisa la mahali ni kiongozi wake, mchungaji.