Skip to content

Mchungaji ni Ufunguo

Ray Mensa Mensah

Miaka michache iliyopita, kanisa moja lilinialika kuzungumza juu ya umisheni kwa siku mbili nyakati za usiku. Nilifurahi, lakini nilikuwa na hisia mchanganyiko. Ni watu wangapi wangejitokeza kwenye kongamano la umisheni siku ya Jumatano usiku? Kwa uzoefu wangu, washirika wachache wa kanisa huhudhuria programu kama hizo. Baada ya kufika, nilishtuka. Sehemu ya kuegesha magari ilikuwa imejaa, na mamia ya watu walijaza jengo hilo.

Askofu alisimulia jinsi ambavyo alijisikia hukumu kutoka kwa Bwana kwa sababu ya kuliacha agizo la kanisa, hata kusababisha hasara ya roho za watu kwenda kuzimu. Alianza kuhubiri juu ya uinjilisti, kufanya wanafunzi, na umisheni. Baada ya wiki kadhaa, alihisi walihitaji mtu aliye na uzoefu zaidi ili awawezeshe zaidi. Kwa hivyo, nilialikwa.

Niliondoka katika kanisa hilo nikiwa nimesadiki jambo nililokuwa nikisema—“MCHUNGAJI NI UFUNGUO!” Washirika wa kanisa hutenda kile ambacho mchungaji anasisitiza. Kwa maoni yangu, wachungaji wanahusika kwenye hali ya watu kutopenda umisheni tunayoiona katika makanisa Afrika na mabara mengine.

Dk. Michael Youssef anaiweka kwa njia hii: “Kama mimbari inavyoenenda, ndivyo na kusanyiko linavyoenenda. Kama kusanyiko linavyoenenda ndivyo na taifa linavyokwenda.” Maandiko yanamwagiza kiongozi “awaandae watu wake kwa ajili ya kazi ya huduma, ili mwili wa Kristo ujengwe, hata sisi sote tufikie umoja wa imani na kumfahamu sana Mwana wa Mungu, hata kuwa watu wazima, hata kufika kwenye cheo cha kimo cha utimilifu wa Kristo” (Efe. 4:12-13). Kwa hiyo wachungaji lazima wajenge utamaduni huo wa kimishenari na kuwatayarisha washirika wa makanisa yao, kama jambo la dharura, kufanya wanafunzi na kupeleka Injili hadi miisho ya dunia.

Ingawa kwa sasa ninahudumu kama mkurugenzi wa shirika la kimisheni, kwa neema ya Mungu, nimechunga makanisa nchini Ghana, Botswana, na Namibia. Ninaelewa mashinikizo na changamoto zinazowakabili wachungaji; walakini, hicho sio kisingizio cha kuwa mtazamo wa kutazama ndani tu. Utume wetu ni wa kimataifa. Bwana wetu Yesu alituamuru, “Nendeni mkafanye mataifa yote kuwa wanafunzi” (Mt. 28:19-20).

Kwa muhtasari, wachungaji lazima wakamate maono ya uinjilishaji wa ulimwengu, kisha waingize maono hayo katika kusanyiko lao. Washirika wataitikia kwa kuchukua hatua katika Yerusalemu zao, Yudea, Samaria, na sehemu za mbali zaidi za ulimwengu. Kisha mchungaji anawaongoza kuunda sera ya umisheni ambayo itaathiri kila idara ya kanisa—watoto, vijana, wanawake, wanaume, kwaya, wahudumu, vyombo vya habari, n.k. Sasa umisheni unakuwa kiini kwa kila mtu anayehusika katika maombi, kutoa na kwenda. . Ninaomba hili lifanyike katika makanisa kote Afrika na kwingineko. Bwana wa Mavuno atumie toleo hili la AfriTWENDE kwa kusudi hilo.

Vyanzo: Lemons, J.D. The Pastor as the Missional Church Architect. Doctoral Thesis. Asbury Theological Seminary, 2007.

Ray Mensa Mensah ni Rais wa AfMA na hapo awali alikuwa Rais wa Chama cha Wamisionari wa Kiinjili wa Ghana (GEMA). Ana shauku juu ya uhamasishaji kamili wa makanisa kwa ajili ya umisheni ambapo kila mshirika anahusika katika Agizo kuu.

Other articles and resources from around the web on this topic: