Wito wa Umishenari na Wasiwasi wa Familia
MASWALI MAGUMU NA MAJIBU YENYE KINA
Umeitwa kutumika kama mmishenari, lakini wasiwasi wa kifamilia kukuvuta unatishia kwenda njia nyingine. Je, unatokaje kwenye hiyo njiapanda? Tumekusanya ushauri kutoka kwa viongozi wa umisheni ili kushughulikia baadhi ya masuala ya kawaida ya familia ambayo hujitokeza unapoamua kutumika kama mmishenari.
Swali: Nimeitwa kuwa mmishenari katika nchi ya mbali, lakini wazazi wangu ambao kwa sasa ni wazee wanahofia maisha na usalama wangu. Pia wanahitaji uwepo wangu na msaada wa kifedha kutoka kwangu. Wanapendelea nisiende. Je, ninashughulikiaje wasiwasi wao na kupata baraka zao?
Hili ni swali la kumtii Mungu na kuwatii wazazi. Huwezi kuliasi Neno la Mungu linalosema, “Yeye aipendaye nafsi yake ataiangamiza, lakini yeye anayeitoa kwa ajili ya Bwana ataipata” (Yn. 12:25). Wakati huo huo, huwezi kuwapuuza wazazi wako na kuondoka kwenda kwenye eneo la umisheni. Kuwatii na kuwaheshimu wazazi ni sehemu ya injili, na pia ni tendo la ibada.
Wasiwasi walio nao wazazi wako wazee ni wa kweli, lakini unamtumikia Muumba wa ulimwengu mzima, naye anaweza kukulinda wewe na familia yako. Wasaidie waelewe kwamba Mungu ndiye anayetuangalia na kutuweka salama. Watie moyo wakusaidie kwa kuombea usalama wako. Hata kama mabaya yatatokea na ukafa kwenye eneo la umisheni, ni bora kufa ukiwa unamtii Bwana kuliko kufa ukiwa haumtii. Ipe familia yako ushahidi wa kivitendo unaoonesha kwamba hutaacha kuwa mwanagalifu na maisha yako. Waambie kuhusu ujuzi na mafunzo ambayo umepata ili kujilinda ikiwa uko hatarini. Wahakikishie kuwa teknolojia itakufanya uendelee kushikamana nao. Wasiliana nao kwa bidii, hata ikimaanisha kusafiri hadi mahali unapoweza kupata mtandao mzuri.
Biblia inasema tusipowatunza wa nyumbani mwetu, sisi ni wabaya kuliko wasioamini. Hata tukiwa katika eneo la umisheni au la, ni wajibu wetu kuwatunza; kutumikia kama mmishenari haimaanishi kukataa wajibu huu. Tafuta mwongozo wa Mungu na uweke pamoja mipango halisi ya kushughulikia mahitaji yao. Unaweza kupanga na viongozi wako wa umisheni kuhusu kupata usaidizi kwa ajili ya kuwatunza, au kupata mtu wa kuwatunza ukiwa mbali. Ikiwa wazazi wako bado wana msimamo mkali, tafuta viongozi wa Kikristo wanaoheshimika ili kuzungumza nao. Omba katika hatua hizi zote, na uwe na subira. Hakikisha kwamba wazazi wako wana amani ipasavyo kabla ya kuondoka kwenda katika eneo la umisheni.
Swali: Ndugu zangu walioko kijijini walichangia kufadhili elimu yangu hadi ngazi ya chuo kikuu kwa sababu nilikuwa mwanafunzi niliyeonesha matumaini. Walitarajia nipate kazi nzuri baadaye na niweze kuwatunza ndugu walio wadogo zaidi wa familia yetu. Sasa ninahisi kuitwa kuwa mmishenari na sina budi kuomba msaada wa kifedha mimi mwenyewe ili niweze kufanya kazi ya umisheni. Je, nisaidie familia yangu au niitikie wito?
Itikia wito wa Mungu (Mt. 6:33). Biblia inatuamuru tuwatunze ndugu zetu, lakini tarajio hilo la familia halina uhalisia. Je! kuna uhakika gani kwamba baada ya shule, utapata kazi ambayo inalipa vya kutosha kumtunza kila mtu? Unaweza pia kuanzisha familia yako mwenyewe.
Hii haimaanishi kwamba usiizingatie familia yako. Bado unaweza kuwatunza kwa kuwaombea, kuwapa ushauri mzuri (sio mara zote kuhusu pesa pekee), na kuwapa mahitaji ya kimwili na ya kifedha. Kwa maombi fanyia kazi mchakato huo, na wafahamishe kile unachoweza kufanya. Labda unaweza kumtunza ndugu mmoja amabye ni mhitaji au tegemezi kwa takriban miaka mitano, au wawezeshe baadhi yao kuanza biashara au kupata kazi au kujifunza ufundi. Kwa heshima, wape uhakika kwamba utafanya kile ambacho Biblia inakuagiza kufanya, lakini pia wajulishe kuwa huwezi kumtunza kila mtu.
Waonyeshe kwamba umisheni ni wito unaostahili. Wakati mwingine mtazamo wetu wenyewe wa kizembe katika kuwasilisha kazi ya umishenari hutoa mvuto usiofaa na kuwafanya wawe na wasiwasi. Bwana anasema mtenda kazi anastahili ujira wake. Waeleze kwamba utalipwa; unaweza usijue jinsi gani, lakini utapata thawabu yako. Tembea kwa unyenyekevu ukipitia ngazi zote za mamlaka katika familia yako, na ombea mchakato mzima.
Swali: Watoto wetu walizaliwa na kukulia katika eneo la umisheni la ugenini ambako walijifunza lugha na desturi za kundi (kabila) la watu tofauti. Mwingiliano wao pekee na wanafamilia wengine umekuwa ni kupitia mikutano michache ya mtandaoni. Tunajiandaa kuwapeleka nyumbani kwa mara ya kwanza baada ya miaka 15. Tunawezaje kufanya uwe wakati wa faraja na wa kuridhisha kwao na kwa familia nzima?
Tafuta kujua kama kuna wanandoa wengine wako katika hali kama hiyo na jadili ni nini ambacho wamegundua kinachoweza kuwa cha msaada. Wakati huohuo, watayarishe watoto mapema kuhusu mambo ya kutarajia mnapoenda kuwatembelea ndugu huko nyumbani. Jambo moja ambalo linaweza kusababisha maumivu kwa familia huko nyumbani ni pale watoto wa wamishenari wanapokuwa hawawezi kuzungumza lugha ya nyumbani. Huenda familia ikahisi kwamba utamaduni wao unasahauliwa au unawekwa kando kwa ajili ya wengine. Ili kusaidia katika hali hiyo, wafundishe watoto wako salamu, ishara, na maneno yanayofaa kuongea na babu na bibi na ndugu wengine wa familia. Zungumza nao kuhusu utamaduni wako—chakula, lugha, mazingira ya familia, shughuli za kiuchumi—mambo mazuri na mabaya ili kuepuka mshtuko wa kitamaduni.
Isaidie familia yako kule nyumbani kuelewa kwamba watoto wako ni watoto wa wamishenari, kwa hivyo huenda mwingiliano wao nao usiwe rahisi. Unaweza pia kuelekeza familia yako kuhusu mazingira ambayo watoto wako wamekulia, ili waweze kuwachukulia na kuwasaidia.
Mvutano kati ya wito wa kimishenari na masuala ya familia ni jambo la kawaida kwa wamishenari wa Kiafrika. Ukijikuta uko katika hali hii, hauko peke yako. Peleka haja zako mbele za Bwana kwa maombi na utafute ushauri wa kimungu na kutiwa moyo kutoka kwa wale wanaoelewa eneo hilo. Usisite kuomba msaada kutoka kwa ndugu wa kiume na wa kike katika Kristo wanaoweza kukusaidia. Mungu alijua utakabiliana na nini akikuita. Mwamini yeye akusaidie kulitii Neno lake kuhusu wito wako na wajibu wako kwa familia yako. Inaweza isiwe rahisi, lakini Mungu ni mwaminifu.