Skip to content

Wito wa Kimishenari na Familia Kutumia Falsafa ya ‘Ubuntu’

Timo AfriTWENDE

Je, ni lazima mmishenari aitelekeze familia yake ili aitikie kiukweli wito wa Mungu wa kuwafikia waliopotea? Katika Bara lote la Afrika, kizazi kipya cha wamishenari wa Kiafrika kinaenda kwenye maeneo ya umisheni, na familia zao hazielewi kabisa sababu zinatolewa kila wakati. Inaweza kuonekana kuwa ni ubinafsi, hasa ikiwa familia ilijitoa muhanga katika kusomesha na kulea huku ikitarajia thawabu baadaye.

Wito wa umishenari Wengine wameitwa katika umisheni kwa njia ya ajabu kama vile ilivyomtokea Paulo huko Dameski. Kwa wengine, ni msukumo unaoongezeka tu unaoonesha kwamba Mungu anataka mwelekeo tofauti kwa ajili yao. Bila kujali njia ambayo mtu au wanandoa hatimaye wanatambua kwamba Mungu anataka waende mahali na kutumika kama wamishenari. Hili linapaswa kuthibitishwa na washauri wa kiroho wanaoaminika na waliokomaa.

Kwa wakati huu, familia inaarifiwa kuhusu uamuzi huo, ambao unaweza kusababisha uthibitisho wa hofu mbaya zaidi walizonazo: mtoto wao atakuwa ombaomba, anaweza kuuawa katika nchi ya kigeni, au kupata watoto ambao hawatajua kamwe babu na bibi zao. Uwekezaji wao huo wa awali kwenye elimu sasa unaonekana kuwa si kitu. Kwa bahati mbaya, mchungaji wa kanisa la mahali wakati mwingine anaweza kuwa mojawapo ya vikwazo vikubwa kwa mmishenari, kwa madai kuhusu mahitaji ya huduma mahali walipo, kutilia shaka wito, au hofu yake mwenyewe kuhusu pesa kuondoka kanisani kwenda nchi ya kigeni. Majibu haya yanahuzunisha kwa mtu ambaye tayari anahangaika, labda kwa miaka mingi, kuhusu mipango ya Mungu ya umisheni kwa ajili yake.

Ubuntu na umisheni

Hebu tuangalie njia mbadala kwa kutumia falsafa ya Kiafrika ya Ubuntu. Inahusiana na msemo wa Kizulu “Umuntu ngumuntu ngabantu,” ambayo ina maana kwamba mtu ni mtu kupitia watu wengine. Je, hatuwezi kutumia hili kwa wito wa umishenari? Je, inawezekana kwamba Mungu ameelekeza wito huo kwa mtu binafsi na jamii inayomzunguka?

Vipi ikiwa mafanikio ya umishenari yatachukuliwa kuwa ni mafanikio ya jamii nzima badala ya mafanikio ya mtu mmoja ambaye anafanya kazi katika shamba la mavuno (eneo la umisheni)? Hebu tupige picha ya jamii inayosikia wito wa Mungu wa wapendwa wao. Wanaomba kwa ajili ya uthibitisho wa wito wao, wanahakikisha kwamba wameandaliwa kwa mafunzo ipasavyo, na wanasaidiwa kiuchumi vyema wanapokuwa wakihudumu katika eneo la umisheni. Wanamkaribisha mpendwa wao anaporudi nyumbani na kumtia moyo anapojitayarisha kurudi shamabani. Ndugu wanakusanyika karibu na wanafamilia ambao, wakati mmishenari hayupo, wanahitaji msaada. Hii haingekuwa udhihirisho halisi wa Ubuntu? Soma jinsi ambavyo familia na jamii ya Grace* walivyoweza kufanya vilevile.

Simulizi ya Grace

Nilipowajulisha wazazi wangu kwa mara ya kwanza kuhusu wito wangu wa umishenari, baba yangu alitabasamu. Mama yangu alisema, “Ni pendeleo kumtumikia Bwana.” Hawakuwahi kuhoji nia yangu wala kunivunja moyo. Kulikuwa na nyakati ambazo sikuwa na uhakika kuhusu mapenzi ya Mungu, lakini sikuzote walikuwa tayari kuzungumza na mimi na kuomba pamoja nami nilipohitaji.

Kabla sijaja kwenye eneo la umisheni niliunda kikundi cha maombi ili kuniombea kila wiki. Wazazi wangu walishiriki mfululizo. Kaka yangu aliliratibu kundi hili baada ya mimi kwenda shambani. Niliacha kazi yangu ili kujitayarisha kwa ajili ya kazi ya umishenari, na wazazi wangu katika uzee wao walinihifadhi kwa mwaka mzima. Hawakuwahi kulalamika juu ya hali yangu ya kutokuwa na uwezo wa kusaidia katika kukidhi mahitaji ya familia. Badala yake walinipa kiasi kikubwa cha pesa kwa ajili ya eneo la umisheni.

Niliacha kazi yangu ili kujiandaa kwenda katika maeneo ya umisheni, na wazazi wangu wa wazee tulienda pamoja nao kwa muda wa mwaka mmoja. Walinihudumia vizuri kwa mahitaji yangu na hawakuwahi kulalamikia hali ya kutokuwa na uwezo wa kukidhi mahitaji ya nyumba. Bali walinipa kiwango fulani cha fedha kwa ajili ya kujikimu nikiwa katika huduma.

Takriban watu 80 walihudhuria katika siku ya ibada yangu ya kutumwa shambani. Familia yangu yote ilikuwepo—wazazi wangu, kaka yangu, dada yangu, mume wake na watoto wao watatu. Marafiki zangu, wanafunzi wenzangu wa zamani, washirika wa kanisa, wafanyakazi wenzangu wa zamani, na viongozi wa umisheni pia walikuwepo. Walizungumza maneno ya uthibitisho juu yangu na kunibariki. Wanandoa fulani ambao ni wamishenari walinipa begi. Rafiki mmoja alikuja nyumbani kunisaidia kupanga mizigo yangu. Mmiliki wa biashara mmoja aliniongeza kwenye orodha yake ya malipo ili kunitumia pesa kila mwezi kama mmoja wa wafanyikazi wake.

Msaada wa kifedha niliopokea ulinitia nguvu kutimiza wito wangu wa kimishenari. Maneno ya baba yangu katika siku ya ibada ya kutumwa shambani yanaelezea moyo ulioko nyuma ya kila msaada nilioupokea kutoka kwa kila mtu—“Kama vile Mariam, mama yake Yesu, tunahisi kuheshimiwa sana kwamba Bwana alichagua familia yetu kwa kazi hii kubwa.” *https://bit.ly/3NAioi9