Tafutu Uwiano
Chinedu Oranye
Familia ni ya muhimu sana kwa Waafrika. Ukiondoa familia, sisi tunajiona sio watu. Familia zetu zenye wazazi na watoto na zile za wazazi, watoto na ndugu wengine zimeunganishwa, na hali hii mara nyingi huamua maamuzi mengi tunayofanya. Je, hili linaathiri vipi msimamo wetu katika umisheni na kama wamishenari?
Kwanza, Yesu anataka uaminifu wa dhati kutoka kwa wote ambao wanataka kumfuata, wakiwemo Waafrika. Katika Mathayo 10:37, anasema, “Yeye apendaye baba au mama kuliko mimi, hanistahili; wala apendaye mwana au binti kuliko mimi, hanistahili.” Yesu alikuwa wazi kuhusu kipimo cha ufuasi, na wito wa kimishenari huanza na kumalizika kwa kumfuata Yesu. Kama Waafrika, lazima tukubaliane na ukweli huu. Hatuwezi kuruhusu wajibu wetu kwa familia utupokonye haki na fursa ya kumtumikia Yesu. Tumeshindwa wajibu wetu ikiwa tutaacha mapokeo ya familia zetu yabatilishe maagizo ya Yesu ya “kwenda kufanya wanafunzi.”Kumfuata Yesu kutaathiri familia, na wakati mwingine, kunaweza kulazimu kufanya maamuzi magumu. Lakini, utii kwa Kristo ndio kipaumbele chetu cha kwanza.
Kwa upande mwingine, Yesu anawaambia Mafarisayo katika Mathayo 15:5-6, “…nyinyi mwasema, Mtu ye yote amwambiaye baba yake au mama yake, “Kicho chochote ambacho ungepata kutoka kwangu ni wakfu kwa Mungu; hana haja ya kumheshimu baba yake au mama yake.’… mmeibatilisha amri ya Mungu kwa mapokeo yenu.” Yesu anathibitisha umuhimu wa kuheshimu familia. Hakukubaliana na ile dhana ya kwamba ukiroho unapingana na kujitoa kwa ajili ya familia. Yesu alibainisha wazi kwamba kutoheshimu familia ni kutotii amri ya Mungu. Umisheni wa kisasa, kwa bahati mbaya, umetufundisha kwamba kuacha familia ilikuwa ni kigezo cha kumtumikia Mungu; hivyo, vijana wengi wa Kiafrika kwa kizembe wametelekeza majukumu yao ya kifamilia katika harakati za kuokoa mataifa. Mwitikio huu wa kibinafsi na umimi umeziacha familia nyingi za kiafrka katika hali ya uadui dhidi ya Yesu na wito wake.
Tunapatanishaje misimamo hii miwili? Kama Waafrika, lazima tutafute uwiano kati ya kumfuata Yesu, kutumika kwenye umisheni, na kuheshimu familia. Ingawa tumeitwa kuyatoa maisha yetu ili kumfuata Yesu, tunapaswa kuendelea kujitoa kwa ajili ya familia zetu na kuzihudumia. Wakati uaminifu wetu kwa Yesu unapaswa kubaki bila mashaka, kuudhihirisha kwetu huo uaminifu hakupaswi kuchoma madaraja yanayotuunganisha na mitandao ya familia zetu.
Katika toleo hili la AfriTWENDE, fuatilia safari ya Reagan ya upinzani kutoka katika familia yake na hatimaye kukubalika kwake kwao na kuungwa mkono nao. Makala ya Mtazamo inatoa suluhu la Kiafrika juu ya njia panda ya familia ya mmishenari. Akina Mama wa Msaada huko Nigeria wanaonesha jinsi wale walio nyumbani wanavyoweza kusimama katika pengo la wamishenari wanaotumikia shambani. Toleo hili la AfriTWENDE na lisaidie wamishenari na familia zao kuelewana na kusaidiana, na kuutia moyo Mwili wa Kristo kusimama pamoja na wamishenari na familia zao.
Dr. Chinedu Oranye ni Mwalimu wa Biblia kutoka Nigeria, mwandishi, mshauri wa mambo ya uongozi, na mchungaji. Huduma yake imempeleka katika nchi zaidi ya 30, akishirikisha Injili ya Kristo ya upendo na imani kwa waliopotea na kwa Kanisa. Anafanya kazi na shirika la Calvary Ministries (CAPRO) na Haggai International. Ni mme wa Taiwo na wana watoto watatu. chinedu.oranye@gmail.com.