Kumbatia watoto wa wamishenari wa Afrika mashariki
Daniel Salamu
Jinsi gani tunaweza kuwakumbatia na kuwalea vyema watoto wa wamishenari wetu katika umisheni? Ni kweli wako katika umisheni, lakini wapo si kwa sababu yao, bali kwasababu ya wazazi wao. Imekuwa ni kawaida kwetu kutoa maelekezo kwao na kutarajia watoto kutii bila kuuliza.
Watoto wangu ni wadogo na walizaliwa baada ya mimi na mke wangu kuwa wamishenari. Hawakuchagua maisha haya, lakini siku moja watachagua. Wanaweza kuikubali au kuikataa kazi hii, kutegemeana na jinsi nitakavyowalea. Ikiwa nitamaliza safari yangu ya umishenari leo, na bado watoto wangu hawaoni jambo lolote jema ndani yake, hilo litakuwa jambo la kukatisha tamaa sana. Badala yake, nataka kuwapa urithi usio na mashaka. Swali la kujiuliza ni: kama wazazi tunawezaje kuishi maisha yenye kuwavutia watoto wetu na kuwapa shauku ya kufuata nyayo zetu?
Nimejifunza kwamba mambo madogo madogo yana umuhimu sana. Sisi watu wazima, tunadhani baadhi ya mambo hayana maana, lakini kwa mtoto yana maana kubwa. Kwa mfano, nilipanga kufanya mkutano muhimu na timu yetu kwenye nchi jirani tarehe 16 ya mwezi. Hata hivyo tarehe 15 ya mwezi huo ilikuwa siku ya kufunga shule kwa mwanangu. Nilisitisha safari na mkutano kwa sababu sikutaka kusafiri siku hiyo muhimu. Nilitaka kuwa pamoja na mwanangu wakati wa hafla au sherehe yoyote na watoto wengine. Uwepo wetu kwenye wakati huo huleta matokeo kwa watoto wetu kwa njia ambayo hatuwezi kujua mpaka baada miaka kadhaa ijayo.
Lazima pia tuwe na nia ya dhati kwa watoto wetu ikiwa tunataka kuona hatimaye umisheni wa kiafrika ukistawi. Ikiwa tutafanya umisheni vibaya, wanaweza kukwambia, “Wewe ndiye uliyechagua kazi hii, sio mimi,” na wanaweza kuacha. Lakini ikiwa wataona kile ambacho wazazi wao wanafanya na kuchagua kumfuata Mungu, basi tutakuwa tukiinua kizazi kipya cha wamishenari na wafadhili wa umisheni. Hata kama hawatakuwa wamishenari moja kwa moja, wataipenda kazi hii na watakua watetezi na wafadhili wa Utume Mkuu.
Tukumbuke jinsi Yesu alivyokwenda Misri wakati fulani alipokuwa mchanga na kipindi cha utoto wake. Baba yake wa mbinguni alimwagiza baba yake wa duniani Kwa njia ya ndoto Yusufu, akimbilie huko. Akiwa na umri wa miaka 12 tunamwona Yesu hekaluni, familia yake ikiwa imerudi Israeli. Labda tunaweza kufikiria jinsi miaka hii ya awali katika ukuaji wake ilivyotumika na utamaduni wa kigeni ulivyoathiri maendeleo ya awali, ufahamu wake wa dunia nzima, na moyo wake kwa watu waliopotea kwa mataifa yote. Ninaamini maisha haya ya umishenari ni maisha bora zaidi ninayoweza kuwapa watoto wangu kwa sababu Mungu aliita familia yangu yote na watoto wakiwa wamejumuishwa. Siku moja nataka watoto wangu waseme, “Baba yangu wa mbinguni na baba yangu wa duniani hawakufanya makosa.”
Katika toleo hili, utasikia kutoka kwa Mkurugenzi wa Ofisi yetu ya Afrika Mashariki, baadhi ya changamoto na Baraka za kuwa mtoto wa mmishenari, utasoma jinsi ya kufanya mabadiliko mazuri kwa watoto kwa kutumia njia ya maridhiano, uhakika na kuangalia mambo yajao, na utasikia habari za mabinti wawili ambao ni watoto wa wamishenari, Baraka na Furaha, ambao hivi leo wanastawi. Maombi yangu ni kwamba utakuja na mtazamo mpana kwa watoto hawa na hata utajitolea kuwaombea na kuombea umisheni kwa ujumla.
Daniel Salamu ni Mkurugenzi wa Ofisi ya SIM iliyoko Afrika Magharibi, ambayo huhamasisha na kutuma wamishenari kutoka mataifa 16. Danieli na mkewe ni wazazi wa WWW watatu: Hadriel, Kirsten-Aurora na Gordon-Bill. Yeye anatoka Nigeria na kwa sasa anaishi Ghana baada ya kutumika kwa zaidi ya miaka 8 nchini Burkina Faso.