“Safari moja ilibadilisha kila kitu” – nyakati za wamishenari

Nilitumia muda mwingi katika maombi na kutafuta ushauri kutoka kwa waumini waliokomaa, na ilikuwa wazi kabisa kwamba Bwana alikuwa ameniita kweli ili niache kazi yangu na kumfuata.
Hata hivyo, Nilitaja majukumu yangu ya familia na visingizio vingine vyenye mashiko.Wakati wowote msukumo wa wito ulipokuja, nilijikumbusha upesi juu ya upumbavu wa kuacha kazi yenye mshahara mnono ili kumwamini “mtu fulani” kwa ajili ya kunipatia mahitaji. Visingizio vya siri vilikuwa ni kupoteza heshima ya kijamii ya daraja la kuwa miongoni mwa tabaka la wafanyakazi. Nilijiuliza, “ikiwa nitaacha kazi yangu ni nini kitatokea kwa watoto wangu, mke wa ujana wangu, wazazi wangu ambao ni wazee na wale wote wanaonitegemea?” Haya yalikuwa maswali muhimu kwangu.
Safari moja ilibadilisha kila kitu na kunifanya nijisalimishe kwa Bwana. Ilikuwa ni usiku mtulivu, wenye upepo. Nilikuwa ndani ya basi nikisafiri kurudi nyumbani baada ya kutoka kuwatembelea wazazi wangu waliokuwa katika jiji lingine. Nikiwa nafurahia safari kwenye basi, nikisikiliza muziki, nikiwa nimefunga mkanda, nilipitiwa na usingizi mzito wa ajabu. Ghafla niliamka nikisikia mayowe na vilio vya kutisha, kelele na vilio vingi na nikawaza pengine nilikuwa na ndoto mbaya. Kumbe, tulikuwa tumepata ajali mbaya sana ya barabarani! Basi lilikuwa limepinduka juu chini na nilikuwa nikining’inia hewani, bado nimefungwa na mkanda kwenye kiti changu; karibu yangu, kulikuwa na majeruhi wengi na damu ilikuwa kila mahali. Vitu vyangu binafsi vilipotea (au kuibiwa) na baada ya kutoka nje ya basi, nilisimama na kutazama abiria waliojeruhiwa vibaya wakipelekwa hospitalini kwa ambulensi (magari ya wagonjwa).
Licha ya kuwa mtaalamu wa Afya, sikuwa na nguvu za kusaidia, kwani mimi mwenyewe nilikuwa na mshtuko. Wakati huohuo, maswali yalisikika masikioni mwangu yakisema: ni nini kingetokea kwa watoto wangu, mke wangu na wazazi wangu wazee na wale wote wanaonitegemea ikiwa ningekufa katika ajali hii mbaya? Je, heshima na cheo/hadhi ya mfanyakazi kwenye jamii vingewafaa hata kidogo?
Hili lilitosha kunifanya niutikie wito wa Mungu na nikanyenyekea kwake: Aliniepusha na ajali hiyo kama onyo. Nilipeleka barua yangu ya kujiuzulu kazini na pia nilimjulisha mke wangu. Nilipowaambia watu wangu wa karibu kuhusu uamuzi wa kuacha kazi, hawakufurahishwa. Waliniuliza swali lile lile: “Ni nini kitatokea kwa familia yako na wale wote wanaokutegemea?” Wengine walidhani kuwa ajali ilikuwa imeathiri ubongo wangu na nilikuwa nafanya uamuzi wa ajabu kwa sababu ya kiwewe.
Miaka tisa baada ya kuvunjwavunjwa na kufanywa upya na Bwana, tunamtumikia kama wahamasishaji wa kitamaduni nchini Lesotho
-Levi “Kgotso”, mhamasishaji wa Malawi nchini Lesotho