fbpx Skip to content

“Nilichukua vidonge mikononi mwangu” – nyakati za wamishenari

Sehemu ya kwanza kati ya tatu:

Nawasalimu wote katika jina la thamani la Yesu Kristo.

Ninaona kuwa ni faida kubwa kukushirikisha jinsi nilivyokutana na Bwana.

Nilikuwa na maumivu ya moyo yasiyoweza kuponywa kulingana na Biblia (Yeremia 17:9). Nilikuwa na umri wa miaka minne pale nilipofiwa na mama yangu na nilihisi utupu maishani mwangu. Hadi kupelekea na kulazwa hospitali. Daktari akasema wamegundua kuwa nilikuwa na tatizo la moyo na hakuna wanachoweza kufanya isipokuwa kunirudisha nyumbani. Bibi yangu, ambaye alinilea, ndiye alinieleza haya nilipokuwa mkubwa.

Hata miaka mingi baadaye, bado nilikua nahisi utupu ndani yangu. Baba yangu alioa mke mwingine, na alipokuwa hayupo kwa sababu ya kazi, mama yangu wa kambo hakunitendea sawa na watoto wake halisi. Ilipeleka hadi kuacha masomo na kuanza kufanya kazi ili kujikimu kimaisha. Nilifanya mambo yale ambayo vijana walifanya, nikifikiri kwamba kitaziba pengo ndani yangu, lakini niligundua kuwa ni pengo kubwa lisiloweza kuziba, sikuwa na upendo wa kutosha. Nilianza kuwa mkatili na kupenda kucheza michezo ya mitaani. Furaha yangu kubwa ilikuwa ni kulipiza kisasi kwa ndugu zangu wa kambo. Kwa bahati mbaya, hata hili pia halikuziba pengo ndani yangu. Kwa sababu ya jeuri yangu, nilishtakiwa na watu na nikafungwa gerezani. Tangu hapo sikuona sababu ya mimi kuzaliwa duniani na nilichanganyikiwa zaidi baada ya haya yote kutokea. Baada ya kumaliza kifungo changu, nilirudi kwenye jamii lakini baba hakuniruhusu kuishi nae tena.

Kutokana na haya yote, watu walionizunguka wakawa mbali nami. Kwa bahati nzuri bibi yangu alikuwa bado yupo na alikuwa ananiombea na kunitia moyo kila mara kuwa Mungu yupo na ananipenda. Hata hivyo, nguvu ndani yangu ya kuwa na imani juu ya mambo hayo ilizidi kufifia kwa kadri ya miaka ilivyoenda.

Siku moja, karibu saa 10 alfajiri nikiwa pale nyumbani, nilizidi kukata tamaa na nilifikiri na kuona kuwa hakuna sababu ya mimi kuishi tena kwenye dunia hii. Kulikuwa na dawa zilizobaki kwenye sanduku langu ambazo zilibaki wakati wa matibabu yangu nilipokuwa mtoto. Nilifunga milango yote nikachukua kalamu na kuandika barua ya kuwaaga bibi na baba yangu. Pia niliandika jina la mpenzi wangu, ambaye nilimpenda sana, lakini pia na yeye alikuwa ameniacha. Niliongeza maandishi kwenye kioo kidogo kilichokuwa ukutani kwa kutumia dawa ya meno ujumbe huo ulikuwa kwa ajili ya wadogo zangu. Nilikusanya vidonge mikononi mwangu, nilipanga kuvimeza vyote mara moja. Nilipokuwa kwenye harakati za kumeza vidonge hivyo, nikapiga jicho na kuona redio ndogo iliyokuwa mezani iliyokuwa imeishiwa na betri na haikufanya kazi kwa wiki nzima kwasababu hatukuweza kununua betri mpya. Ghafla, ikawaka na kulikuwa na wimbo ambao ulionekana moja kwa moja unasema na mimi na kuniambia nini cha kufanya: “Je, umechanganyikiwa na kutaka kujiua?. Mpokee Yesu Kristo kwenye maisha yako, maana yeye ndiye uzima wako. Hakuna cha kingine cha kutumainia katika maisha haya, mkubali kuwa Bwana na Mwokozi wako.” Magoti yangu yalianza kutetemeka na machozi yalinidondoka. Nilipiga magoti chini na kumwomba Mungu. Kuanzia hapo nikawa karibu na bibi yangu. Aliniongoza sala na nikampokea Bwana, na nilihisi kubarikiwa. Nilihisi lile pengo kubwa ndani yangu lilikuwa limezibwa.

Ushuhuda kutoka kwa Tsimavandy Daniel, Mmishenari wa Malagasi

picha na AIM Stories

share
share
Instagram
contact us
contact us
contact us