“Swali lake lilitutoa machozi”- nyakati za wamisionari
Ninamtumikia BWANA nikiwa ni mmisionari kati ya watu wahamaji wa Turkana kaskazini mwa Kenya, pamoja na kua mwenyeji wa wakimbizi wengi kutoka zaidi ya mataifa 20 katika kambi ya wakimbizi ya Kakuma iliyokua karibu. Imekuwa yenye kustaajabisha kuona BWANA akibadilisha watu kupitia mahubiri na kufanya uinjilisti.
Wakati fulani huko nyuma nilipata fursa ya kuchukua injili na kusambaza chakula kwenye kijiji kilichoitwa Nawountos. Rafiki yangu Lee ambaye alikuwa na pesa na alikuwa na mzigo wa kulisha maskini, alibeba chakula huku mimi nikibeba Biblia yangu. Alitania, “Eugene atabeba mkate wa uzima na mimi nitabeba chakula cha kimwili kuwalisha wenye njaa.” Na kwa hivyo tuliendesha gari kilomita 80 kwenye barabara mbaya isiyo na usalama kwenye Toyota Hilux hadi kijiji cha mpakani.
Tulipokua njiani, tuliogopa kukutana na wavamizi waliovamia jamii yao waziwazi. Waturkana kutoka upande wa Kenya kuvuka mpaka na kuvamia jamii za Waganda na kwa upande wao jamii za Waganda wangevuka hadi Kenya na kuvamia. Uvamizi ni shughuli hatari kwa sababu inahusisha kuwahamisha wanakijiji, mauaji, na kuiba. Tulifika katika kijiji hiki na kukusanya watu na tukaanza kuwagawia chakula watu wapatao 200 walioketi karibu na mti. Baadaye, nilikuja kushirikisha injili. Nilifungua Biblia yangu na kushirikisha Neno la Mungu kwa muda wa dakika 30 hivi kisha mtu fulani akainua mkono wake na kuuliza swali. Katika jamii za wafugaji au wahamaji, ni sawa kiutamaduni kukatiza mazungumzo au hadithi au mtu akizungumza na kuuliza maswali. Mwanaume aliyekuwa ameketi nyuma aliinua mkono wake na kuuliza swali. Unaona, nilikuwa nimewaambia kwamba injili ya Yesu Kristo ilikuwa imekuja miaka mingi iliyopita katika jiji kubwa la Nairobi na miji mingine. Kwa hiyo mtu huyu akauliza, “Ikiwa injili hii, ujumbe huu mzuri unaotuletea leo, ulikuja Nairobi miaka mingi iliyopita na kufika katika jiji la Eldoret na miji mingine ya nchi hii, nani ambao walichelewesha ujumbe huu kufika kwetu ili kwamba tuweze kuamini?”
Nilimtazama Lee akanitazama tukashindwa kujibu; tuliitikia kwa machozi. Tuliondoka katika kijiji hicho baada ya sala ya mwisho na swali hili lilikuwa likivuma akilini mwetu. Lee alikuwa anaelekea uwanja wa ndege, kurudi Amerika, akalia huku akisema, “Mbona naenda Amerika wakati kuna vijiji vya mpakani mwa Kenya na Uganda ambavyo havina kanisa na watu wanaoishi milimani ambao hawajawahi kusikia injili?” Hatimaye aliondoka na nikaachwa nyuma na swali hili daima limekuwa nyuma ya akili yangu: “Ni nani aliyechelewesha ujumbe huu wa Yesu kufika kwetu?” Ni changamoto kwetu; ni changamoto kwa kila mtu ambaye ni mkristo, ambaye amepokea nuru. Je, tunaweza kuwa tunachelewesha ujumbe kwa mtu? Je, kunaweza kuwa na mtu wa karibu ambaye anahitaji kusikia tunapochelewesha, tukichukulia kwamba wamejua, na huku tukiyaweka kwetu?
Lakini nina habari njema. Ninaendelea kuombea kijiji na baada ya miaka 9 hivi nilirudi kijijini hapo mwaka jana na kukuta kanisa limepandwa, na injili imewafikia watu wa kijiji cha Nawountos.
-Kutoka kwa Eugene Mbatha, mmisionari kutoka Kenya