“Mungu, tuokoe!” – nyakati za wamisionari
Tulichukua timu ya wageni kufanya huduma katika kisiwa kilicho karibu na pwani ya Msumbiji ambapo baadhi ya washiriki wa misheni yetu walikuwa wakipanda makanisa. Ilichukua masaa nne kufika kisiwani kwa jahazi. Sehemu ya kwanza ilikuwa mbaya kwani ndipo mto ulipounganika na bahari, lakini safari iliyobaki ilikuwa sawa. Wakati wa kurudi, hata hivyo hatukuwa na safari isiyokua na mkwamo kama hiyo.
Kawaida majahazi hubeba watu wapatao 15 na ilikusudiwa kuwa timu na mizigo yetu tuu, lakini wasimamizi wa mashua waliamua kuchukua watu wengine pia. Walisema kwamba ilikuwa mashua pekee siku hiyo na watu walihitaji kwenda wote pia. Hatukuweza kubadilisha ratiba yetu, kwa hiyo sote tukaingia kwenye mashua na kuondoka.
Kwa kawaida, watu hao walikuwa wakipiga makasia hadi sehemu fulani, kisha walipofika mahali ambapo mto ulikutana na bahari, waliweka tanga kwa sababu ilikuwa ngumu sana kupiga makasia. Hata hivyo, kwa sababu mashua ilikuwa imejaa kupita kiasi, walingoja kuweka matanga hadi baadaye kidogo. Kisha, ilikuwa ni kuchelewa sana na hawakuweza kuinua tanga, na mashua ilikuwa inaelekea kando.
Vijana hao walikuwa wamechoka sana kwa kupiga makasia kwa sababu mashua ilikuwa nzito sana, na mashua ilikuwa ikienda polepole kuliko kawaida. Kisha maji yakaanza kuingia ndani ya mashua, na ilitubidi sote kutafuta chombo na kuchota maji kutoka kwenye mashua. Ilikuwa ya kutisha na mashua ilikuwa inasukumwa tu na mawimbi. Kila mtu ndani ya mashua alianza kusali na kumlilia Mungu atuokoe, atusaidie kufika pwani. Ilikuwa tukio la kutisha, na wakati hatimaye tulienda ufukweni na kutoka nje, kila kitu kilikuwa kimelowa. Watu walikuwa wamelowa, mikoba yetu ilikuwa imelowa, Biblia zilikuwa zimelowa, simu zilikuwa zimelowa, kamera zilikuwa zimelowa, kila kitu kilikuwa kimelowa. Lakini jambo la kuvutia ni kwamba tulipokuwa kwenye ardhi na tukiwa na ardhi chini ya miguu yetu, hatukujali kwamba mambo yetu yote yameharibiwa. Tulifurahi sana kuwa hai, na tulikuwa tukimsifu Mungu kwa hilo.
-Mmisionari wa Zambia nchini Msumbiji