“Watoto walinipa jina jipya” – nyakati za wamishenari

Siku ya kwanza, mpango kazi wa somo langu (lesson plan) haukuwa unaenda kama nilivyotarajia, licha ya kuwa nilikuwa nimeuandaa mapema. Sikuweza hata kuona pa kuanzia. Watoto walikuwa wanapiga kelele sana, na haikuonekana kama walikuwa tayari kumpokea mwalimu mpya. Nikamuomba Mungu anisaidie nijue namna ya kuvuta umakini wao.
Ghafula, wimbo mmoja ukanijia akilini: “Panzi kutoka kwenye eneo la dimbwi.” Ndani ya dakika moja, watoto wote walikuwa wamejifunza wimbo huo na wakaanza kuimba pamoja nami. Nikaanza kucheza nao kwa mtindo wangu wa kipekee, nikiwaonyesha jinsi panzi anavyotembea kwenye dimbwi. Ilikuwa hali ya kuchekesha na ya kufurahisha, na watoto wote walijiunga nami katika kutembea na kucheza. Baadhi ya watoto kutoka madarasa mengine walitoka kwenye vipindi vyao na kujiunga na darasa letu, kwani banda letu lililokuwa likitumika kama darasa lilijengwa kwa makuti, na hivyo kurahisisha kuona kinachoendelea na kuwawezesha watoto kuruka kutoka darasa moja hadi jingine bila kizuizi. Tulipotangaza, “Sasa tumemaliza, kila mmoja arudi kwenye darasa lake,” hakuna hata mmoja aliyeonyesha nia ya kuondoka.
Hatimaye, tulilazimika kuwa na darasa moja la pamoja kwa somo la elimu ya dini hadi siku ya kuondoka kwangu. Watoto walifurahia sana vipindi vyangu kiasi kwamba walinipa jina jipya: Mwalimu Panzi (Mr. Grasshopper). Hadi leo, kila ninapopita karibu na shule hiyo — ambayo ipo jirani na barabara kuu — watoto bado hunikumbuka na hunikumbusha kila nilichowafundisha wakati nilipokuwa nao. Cha kuchekesha ni kwamba watoto huangaliana na kusema, “Tazama, Mwalimu Panzi anakuja!” Wakati mwingine ninapotembea kijijini, utaanza kusikia watoto wakiimba ule wimbo kwa sauti, kwa sababu wameniona. Kupitia wimbo huo, niliweza kujenga uhusiano wa karibu sana na watoto, na pia nilijifunza jinsi ya kufanya kazi nao — jambo ambalo limekuwa msaada mkubwa kwenye eneo langu jipya la umisheni sasa.
– Francis Kuntenga, mmishenari wa Kimalawi anayehudumu nchini Msumbiji.