“Maiti zilikuwa zimelala kando ya barabara” – nyakati za wamishenari
Hadithi ya Mmishenari ya ukombozi wa Mungu kutoka kwa magaidi. Wakati Daudi katika Zaburi 23 alisema kwamba “hata nijapopita kati ya bonde la uvuli wa mauti, sitaogopa mabaya, kwa kuwa Wewe u pamoja nami”, ilikuwa dhahiri zaidi kwetu kama familia wakati tukisafiri. Safari ilianza vizuri, tukiondoka eneo letu la huduma hadi mahali papya. Siku ya pili ya safari yetu, tulikosea njia.
Tulikuwa tumepewa maelezo ya barabara gani ya kupita, lakini ramani ya Google (Google map) ambayo sisi tuliitegemea ilitupa njia fupi zaidi bila kutuonya kwamba njia ilipitia eneo la hatari sana kwa shughuli za kigaidi. Tuligundua hatari tulipokuwa tayari ndani kabisa ya barabara huku magari yaliyokuwa yamelipuliwa yakiwa yametapakaa barabarani na maiti zikiwa kando ya barabara.
Tulikuwa tumepoteza mwanga wa mchana, jambo ambalo lilifanya kurudi nyuma kuwa chaguo gumu zaidi kuliko kwendelea mbele kwani tulikuwa tayari tumesafiri kwa masaa kwenye barabara ile ya hatari. Tulikuwa karibu na kutoka eneo hilo ikiwa tungeendelea mbele kuliko kurudi nyuma, hivyo tuliendelea, huku tukiimba, kuomba, na kumsifu Mungu.
Ingekuwa muujiza tusingekutana na magaidi, lakini muujiza mkubwa zaidi ulikuwa kwamba tulikutana nao na wakatuacha tuende.
Baada ya kutuamuru tusimame, tuliwasalimia nao wakaitikia. Waliuliza tunatoka wapi na tunaelekea wapi. Hii ilifuatiwa na ukaguzi na huku silaha zao zimeelekezwa kwetu. Walimwona mke wangu na mtoto mchanga kiti cha nyuma, na kisha mtoto wangu mwingine mdogo wakiume alitabasamu, na wao walitabasamu tena na kumpungia mkono, na kutuambia tuendelee.
Kupitia barabara iliyopandwa na IED (mabomu), baadaye tulipita nakuondoka eneo hili la kigaidi. Maafisa wa serikali ya Kiislamu walitusimamisha. Walipogundua kwamba sisi ni Wakristo, walituambia kwamba lazima tumetumia namna rafiki kwa magaidi, la sivyo, tusingeweza kunusurika.
Hata hivyo, tuliwaambia kwamba ni Bwana wetu Yesu Kristo tunayemtumikia, ndiye aliyetuokoa sisi.