“Kubeba takataka kwa ajili ya injili”- Nyakati za wamisionari
Timu yetu ya muda mfupi kutoka Ghana ilianza kufanya uinjilisti katika vitongoji duni vya Kibera, jijini Nairobi, na na hapo tukakutana na kundi la watu wakifanya usafi pembezoni mwa nyumba zao. Tulijaribu kuwasemesha, lakini hawakutusikiliza na walitukwepa.
Kijana wetu mmoja, aitwae Ralph, alikuwa na wazo juu ya ujumbe wa Paulo wa kuwa kila kitu kwa kila mtu ili kuweza kupata baadhi ya watu. Alimsogelea mmoja wa watu waliokuwa wamesimama karibu na takataka zilizokusanywa kwenye kikapu, na akajitolea kumsaidia kuzitupa. Kijana huyo akamruhusu na kuendelea kufanya nae kazi kwa furaha.
Ralph alibeba kikapu cha takataka kichwani huku maji yakitiririka kwenye shati lake la mikono mirefu. Aliporudi kutoka kutupa takataka, hata wale waliokuwa wamekaa mbali na kumkwepa walimkaribia kumsikiliza atakachosema. Mmoja wao alimuuliza Ralph kwa nini alifanya hivyo. Ralph alijitambulisha, na kuwaeleze jinsi ilivyokuwa muhimu kuwaonyesha majirani wetu wema. Aliwaambia kuhusu upendo wa Mungu kwetu bila kujali tumefanya nini, na jinsi Yesu alivyokufa ili kutuokoa na dhambi zetu.
– Excellent Youth Outreach