MAONI YA MHARIRI UJUZI NA STADI KWA AJILI YA IBADA
Na Mch. Dk. Joshua Bogunjoko
Bwana akanena na Musa, na kumwambia, Angalia, nimemwita kwa jina lake Bezaleli mwana wa Uri, mwana wa Huri, wa kabila ya Yuda; tena, tazama, nimemchagua, awe pamoja naye, huyo Oholiabu, mwana wa Ahisamaki, wa kabila ya Dani; nami nimetia hekima katika mioyo ya wote wenye moyo wa hekima, ili wapate kufanya vyote nilivyokuagiza; yaani, hema ya kukutania na sanduku la ushuhuda, na kiti cha rehema kilicho juu yake, na vyombo vyote vya Hema,’ (Kutoka 31:1-2,6-7).
Watu wengi huona vipawa vyao na ujuzi wao kama tu njia ya maisha ya kawaida ya kujipatia mkate wa kila siku. Kutumia ujuzi wetu kujipatia maisha mazuri, kwa ajili ya familia zetu na kuishi maisha bora ni lengo la kawaida. Hakuna kitu kibaya na kusudi hili. Swali ni kama tumetengenezwa tu kwa ajili ya kufurahia maisha yetu au kwa ajili ya kusudi kubwa zaidi. Je, maarifa na ujuzi wetu ni kwa ajili ya kujipatia kipato au ni kwa ajili ya ibada?
Katika kitabu cha Kutoka, Mungu anamwelekeza Musa kujenga hema mahali ambapo uwepo wake ungekaa na katika eneo ambalo watu wake wangeweza kumwabudu. Kazi hiyo ingehitaji vifaa muhimu vya ujenzi, lakini pia ufundi stadi wa hali ya juu kabisa. Musa angewezaje kupata ufundi stadi huo? Vema, Mungu alikuwa na jibu.
Kujenga Hema la Kibinadamu
Kuna masomo kadhaa kutoka katika kifungu hiki cha maandiko yanaendana na kazi za umisheni wa leo. Kwanza, Mungu ndiye Mwanzilishi wa kazi yote ndani yetu na huifanya kupitia sisi na ndiye mtoaji wa stadi na vipawa – hata vile ambavyo tungeweza kufikiri tumevipata kwa nguvu zetu wenyewe. Kusema kweli Bezaleli na Ohaliabu walifanya kazi kwa bidi ili kuwa mafundi stadi. Hata hivyo, Mungu aliwaambia hakuwaita wao na kuwateua katika kazi hiyo tu, bali pia amewapa uwezo wa kupata stadi hizo: ‘nami nimemjaza roho ya Mungu, katika hekima, na maarifa, katika ujuzi, na mambo ya kazi ya kila aina, (Kutoka 31:3).
Kisha Mungu aliwapa wengine stadi ili wajiunge na kazi hii. Na mwisho, watu wa Mungu walikuwa na moyo wa kutoa vifaa vya ujenzi vilivyohitajika. Bezaleli na Ohaliabu, pamoja na wana wa Israeli walitambua kuwa vipawa vya Mungu na maarifa havikutolewa kwa ajili manufaa yao tu. Vilitolewa kwa ajili ya ibada na kwa kujenga hema la Mungu.
Bwana angali akiwaita watu wenye maarifa na stadi tofauti tofauti ili kutumika katika kazi yake ya mahema ya kibinadamu, yaani makazi ya Roho Mtakatifu. Anawazawadia watu na vipawa mbalimbali vya kiroho na aina zote za maarifa kwa ajili ya kazi hii. Anawatumia wale wenye uwezo katika udaktari wa binadamu, uhandisi, uhasibu, theolojia, elimu, sheria, ujenzi, kilimo, ufundi bomba, uuguzi, kompyuta na nyinginezo! Stadi hizi zimetoka kwa Bwana ili kila mmoja wetu aweze kuzitumia kumfanya Mungu ajulikane. Stadi hizi zinaweza kugeuzwa kwa ajili ya Mwokozi kwa ajili ya wale ambao isingekuwa hivyo wasingeweza kuishi na kufa bila kusikia habari njema za Bwana Yesu.
Mungu anatumia wanataaluma Miaka 21 iliyopita, mimi na mke wangu, Joanna tuliamua kutumia ujuzi na stadi zetu katika udaktari wa binadamu kwa ajili ya kazi ya Mungu ya umisheni ulimwenguni. Tumekuwa tukibarikiwa kumwona Mungu anavyotumia hiyo sadaka ndogo katika maisha ya wagonjwa na familia zao katika umisheni wa kutoa huduma hospitalini katika nchi ambayo watu wake karibu wote ni Waislamu. Tumeona mlango wa injili ukifunguka katika kijiji ambacho asilimia 100 ni Waislamu kwa sababu tu ya huduma hii ya udaktari. Tumeowana vijana wakibadili masiaha na kufanyika kuwa wanafunzi wa Yesu- na sasa wanaipeleka injili kwa wengine.
Watu wengi ambao bado wanaishi bila nuru ya injili hawawezi na hawatawakubali wamishenari wanaofanya kazi kiutamaduni, lakini watu hao wanaweza kumkaribisha mtaalamu mwenye taaluma. Wengi wa waliotuletea sisi injili wenyewe walikuwa ni watu wenye taaluma.
Ujuzi pekee ambao Mungu hawezi kuutumia ni ule ambao haujatolewa kwake kama kitendo cha ibada. Basi leo nasi tutoe vipawa vyetu na stadi zetu kwa ajili ya umisheni wa kidunia.
Mch. Dk. Joshua Bogunjoko, Mkurugenzi wa Shirika la Umisheni la Kimataifa (SIM International)