“Hatukuweza kukihonga kifo” – nyakati za wamishenari

Nilikuwa daktari katika hospitali ya jeshi nchini Ghana, na nilitumwa kwenye jukumu la kulinda amani nchini Côte d’Ivoire, katika hospitali ya Umoja wa Mataifa iliyoko Bouaké. Tulikuwa na daktari wa upasuaji, nami nilikwenda kama daktari bingwa. Zilipotimia wiki tatu baada ya kuwasili, nilikuwa nikisafiri kuelekea kusini, mji mkuu uitwao Abidjan, pamoja na naibu kamanda wetu na dereva wetu, sajenti wa jeshi.
Takriban saa moja kabla ya kufika jijini, gari lililokuwa linakuja upande wa pili lilipasuka tairi, likapinduka mara kadhaa na kuvuka katikati ya barabara—na likaja moja kwa moja kutuelekea. Hakukuwa na muda wa kujihami, isipokuwa kupaza sauti na kusema, “Yesu! Tusaidie!” Kulisikika kishindo kikubwa sana na madirisha yote yakapasuka.
Nilishangaa kujikuta bado nikiwa hai, nikajikagua kuona kama kuna mifupa iliyovunjika. Hakukuwa na hata mmoja uliovunjika—isipokuwa jeraha kubwa kwenye bega. Nilipotazama pembeni, nikagundua kuwa daktari mwenzangu (naibu kamanda) tayari alikuwa amefariki. Dereva alikuwa amening’inia juu ya usukani, akiumia sana.
Niliweza kuomba msaada, na tukamtoa barabarani, lakini niligundua tayari alikuwa amepooza viungo vyote (quadriplegic). Hakukuwa na gari la wagonjwa wala msaada wowote wa haraka. Hatimaye, mtu mmoja alitupatia usafiri kwenye sehemu ya nyuma ya gari aina ya pickup lililobeba magunia ya nafaka. Yule dereva maskini alipata mateso makubwa sana njiani kuelekea hospitalini. Alifanyiwa upasuaji, kisha akahamishwa kwenda Ghana kwa matibabu zaidi, lakini alifariki ndani ya wiki mbili.
Faraja yangu pekee ilikuwa kwamba Roho Mtakatifu alinichochea kuzungumza naye njiani kuelekea hospitalini, na akampokea Yesu wakati tukielekea huko.
Ajali hiyo ilibadilisha kila kitu kwangu, kwa sababu Bwana alikuwa ameninusuru, na nilihisi alinipa uhai kwa kusudi lililokuwa zaidi ya taaluma ya udaktari. Moyo wangu kwa Bwana uliwaka upya kwa nguvu.
Nilihisi kama nimeokoka tena upya — kama mtu aliyerudi kutoka kwa wafu. Mwisho wa mwaka mmoja wa jukumu hilo la kikazi, niliamua kuondoka na kuelekea Canada, nikiwa na hakika kwamba ninaenda kama mmishenari. Tangu wakati huo, Mungu amekuwa akitenda mambo ya ajabu kupitia maisha yetu.
Huwezi kupitia tukio kama hilo na kubaki kama ulivyokuwa. Unaweza kuwa na hadhi na mambo mazuri ya hapa duniani, lakini yote hayo hayana maana. Tulipita mbele ya askari waliotusalimia kwa heshima (Salute), lakini kifo hakisalimu. Tulikuwa na pesa, lakini hatukuweza kukihonga kifo. Tulikuwa madaktari wenye elimu, lakini elimu haikuweza kutuokoa.
Andiko nipendalo zaidi ni Wagalatia 2:20: “Nimesulubiwa pamoja na Kristo, wala si mimi tena ninayeishi, bali Kristo anaishi ndani yangu. Na uzima ninaoishi sasa katika mwili, ninaishi kwa imani katika Mwana wa Mungu, aliyenipenda na kujitoa nafsi yake kwa ajili yangu.”
Dr. Yaw Perbi, mwanachama mwanzilishi wa Send Africa Network katika timu ya kimataifa ya uongozi. Ni mwandishi mwenza wa kitabu cha Africa to the Rest, kiongozi ndani ya harakati ya Lausanne, na pia ni Mkurugenzi wa Kimataifa wa Kwiverr.