“Walikuja kuchota maji” – nyakati za wamishenari

Mnamo mwaka 2023 nilihama kutoka jijini hadi kwenye eneo langu jipya la kazi ya misheni kaskazini-magharibi mwa Msumbiji, kilomita 100 kutoka mji ambao nilikuwa nikiishi na kufanya kazi. Mtangulizi wangu, kutoka Australia, alikuwa amestaafu. Mimi ni wa kabila na lugha moja sawa na watu katika kijiji hicho cha Waislamu, ingawa kutoka ng’ambo ya mpaka wa Malawi. Kwa hivyo, nilidhani itakuwa rahisi kuhusiana nao. Lakini niligundua kuwa waliogopa kuniongelesha, hata kunisalimia! Niliona hofu na mashaka katika nyuso zao.
Nilijaribu kujua ni kwanini, nilishangaa kusikia kuwa wanawaogopa watu wageni kutoka magharibi, wakidhani walikuwa kwenye biashara ya kununua na kuuza viungo vya mwili wa binadamu. Kwa hiyo, pia waliogopa kuhusiana na kila mtu anayefanya kazi na watu wa nchi za magharibi, wakifikiri kwamba nilikuwa nimeajiriwa kuuza sehemu za mwili wa binadamu na mifupa. Wakati huo, uvumi wa kuua watu wenye ualbino pia ulikuwa umesambaa.
Baada ya kuomba kwaajili ya hekima, Mungu alinipa wazo. Nilifahamu ya kwamba wanakijiji walilazimika kutembea umbali mrefu kutafuta maji mtoni au visimani. Kijiji kizima kilikuwa na visima viwili tu. Kulikuwa na maji safi kwenye visima, lakini pampu ilihitajika ili kuyatoa ardhini. Ingawa ilikuwa ghali, niliamua kutoa sehemu ya mshahara wangu wa mafuta wa kila mwezi ili kuweza kupata maji na kuwasambazia pia majirani zangu bila gharama yoyote. Sikujua kama Mungu angetumia hili kutengeneza njia. Mwaka uliofuatia, shirika langu la misheni liliamua kutununulia pampu mpya kabisa ya maji inayotumia umeme wa jua.
Leo hii, majirani zangu wote wameifanya nyumba yetu kuwa kama makazi yao. Kwa miaka miwili sasa, tumekuwa tukitoa maji safi na salama kwa watu wengi kijijini. Maji yamekuwa njia nyingine ya kushiriki upendo wa Kristo kwa wanakijiji, hasa kwa wanawake. Tunazungumza sana kila wanapokuja kuchota maji. Ni vizuri hasa kwamba wanakuja kwa makundi, ambayo inafanya iwe rahisi kushirikishana nao pamoja. Wanaume pia huja kutusaidia kazi za hapa na pale, na tunaitumia kama njia ya kushiriki imani yetu. Sasa wanajua na kuelewa sisi ni kina nani na wamekuwa marafiki wazuri. Maji yamekuwa njia ya kuunganisha mawasiliano. Utukufu kwa Mungu.