fbpx Skip to content

Wajibu Wa Mchungaji Katika Kuanzisha Kanisa lenye Mtazamo Wa Umisheni

By Philip Kofi Tutu

Rev. Philip Kofi Tutu

Kufanya kazi miongoni mwa watu ambao bado hawajafikiwa ni muhimu sana katika kukuza hamasa kwa ajili ya umisheni ndani ya mioyo ya wachungaji na viongozi wa kanisa. Mtu mmoja aliwahi kusema kwamba, hatutakuwa na mzigo kwa ajili ya watu waliopotea mpaka hapo tutakapopata uzoefu unaoitwa “utakatifu wa kutotosheka”. Na hiyo hutokea pale tunapojiweka wenyewe katika mahali ambapo tutajihisi kuwa hatujatosheka- mahali ambapo mioyo yetu itavunjika na itanyenyekea kwa ajili ya waliopotea, mdogo na wa mwisho.

Kuingia kwangu katika umisheni ilikuwa ni pale nilipoanza kutumika miongoni mwa watu wa Dangme, wanaoishi kusini mwa Ghana karibu na mto wa Volta. Niliingia kikamilifu kwenye huduma ya kichungaji mwaka 1981, na kanisa langu lilinituma kutumika kwa waDangme.

Ilikuwa ni huduma ngumu na yenye changamoto. Nilipoenda mara ya kwanza, nilikuwa peke yangu. Niliogopa kwenda pamoja na mke wangu kwenye eneo hilo. Dini ya Voodoo ambayo inaamini sana katika uchawi ilikuwa na nguvu sana katika eneo hilo. Ukiongea kinyume na miungu yao au ibada zao za sanamu, wangeweza kukushambulia. Lakini Mungu alikuwa mwema na alitulinda.

Tulipanda makanisa saba miongoni mwa waDangme na uzoefu huu uliumba hamasa ndani yangu kuwa na huduma ya umishenari. Miaka 10 baada ya kuondoka kwetu, ilikuwa vizuri kuona bado uwepo wa Mungu ulikuwa pale. Tulirudi makao makuu ya nchi yetu ambapo tulihusika na huduma kwenye maeneo ya mijini kwa miaka miwili. Uzoefu wangu wa mwanzo ulinifunza kuwa hakuna kanisa litakalokuwa na mafanikio mpaka litakapokuwa na maono ya umisheni, na kwa hiyo nilidhamiria kuona kila mchungaji anapata fursa ya kimisheni kila mwaka. Safari fupi fupi ni muhimu, na zinapaswa kuhusisha wazee wa kanisa pia. Wanaporudi huwa na mwanga mpya katika macho yao, ili kulihamasisha kanisa kuhusu umisheni na changamoto zake.

Chukua hatua ya kuongoza!

Ni lazima tushirikishe maono kwa ajili ya kazi za Umisheni makanisani mwetu. Hata hivyo, kama unaamini katika kitu fulani lakini hukizungumzii kabisa kitu hicho, hapo kuna tatizo mahali fulani. Na hii yaweza kusababishwa na vikwazo vingi kuinuka vichwani mwao. Vikwazo hivi vinaweza kuwa ni pamoja na mazoea au mapokeo ya kiutamaduni (hivi sivyo tulivyozoea kufanya mambo yetu), mtazamo (hatuko tayari kufanya hili), msimamo wa kimadhehebu (hii siyo sera ya kanisa/dhehebu letu); na vizuizi vya kisiasa (hii inaweza kuwa hatari).

Wakati ambapo makanisa yanapoanza kujihusisha na umisheni, kila kitu hubadilika. Maisha yao ya maombi hubadilika na huanza kuwa na mtazamo mpana katika kumtumikia Mungu kuliko kuangalia mambo yao wenyewe. Wanaona mahitaji yanayowazunguka na mioyo yao huvunjika. Na huanza kuwa huru zaidi kuachilia watu na fedha kwa ajili ya kazi ya Mungu.

Kanisa la Afrika linayo nguvu ya ndani. Baadhi ya makanisa yetu yenye watu wengi hayakupokea misaada kutoka nje. Kwa hiyo, tunaweza kuwatia moyo na wengine; kanisa ambalo limekua kutokana na nguvu ya ndani linawezekana kila mahali.

Nchi za Magharibi zilituma wamishenari ili tuweze kuisikia Injili. Sasa ni zamu yetu kufanya yale yale kwa kutoka ili kuwafikia wale ambao bado hawajamjua Yesu. Afrika isingeweza kusikia habari njema isipokuwa kwa gharama iliyolipwa na wengine. Huu ni wakati wetu wakujitayarisha ili kuwa faraja kwa wengine na kuwa tayari kuhatarisha maisha yetu kwa ajili ya Injili. Tunamtumikia Mungu Mmishenari na Umisheni ndiyo mapigo ya moyo wa wake (Mwanzo 3; Isaya 6; Yohana 3:16). Kuwafikia wengine kwa Injili kutakugahrimu muda wako na fedha yako— inaweza kuwa hata maisha yako. Itakugharimu kila kitu. Lakini wewe NENDA tu! Yesu alikuwa tayari kupata hasara ya vyote, kwa hiyo, tunapaswa kufuata mfano wake. Wachungaji, ninawatieni moyo katika kuongoza, kuelekeza na kuendeleza katika kujenga makanisa yenye afya bora ambayo yana shauku kubwa kwa ajili ya umisheni kote ulimwenguni.

Mchungaji Philip Kofi Tutu, ni Mkurugenzi na Mwenyekiti wa Baraza la SIM huko Madina – Acra, Ghana, na pia ni mwalimu wa wachungaji juu ya uongozi, uinjilisti na umisheni. Philip na mkewe, Janet, wana watoto watano, ambao kwa sasa wana umri wa miaka kati ya 15 na 32.

share
share
Instagram
contact us
contact us
contact us