fbpx Skip to content

Mungu Hakutengeneza Meza; Aliumba Miti

By Mercy Kambura

Trees

Kuna uhusiano gani kati ya hadithi ya Msamaria Mwema na Biashara ya Kimisheni? Au biashara yo yote kwa ujumla? Johnson Asare, mwanzilishi na Mkurugenzi wa kitaifa wa huduma za Markaz Al Biashara huko Tamale, Ghana, anatoa funzo la kutufungua macho kwa kutumia hadithi ya Msamaria Mwema kuhusu mahitaji ya Mkristo katika kufanya biashara na umisheni kwa mafanikio.

Johnson ambaye hupenda kujiita mtumishi mkuu wa huduma, anajua vizuri umuhimu wa biashara na umisheni. Kabla ya kuingia katika huduma, Johnson alikuwa mwalimu wa sayansi, na aliongozwa kumpokea Yesu Kristo na mishonari kutoka shirika la SIM, na amekuwa kwenye kazi za misheni kwa miaka 30. Hivi leo, yeye ni mhadhiri wa masomo ya Biashara ya Kimisheni katika vyuo. Pia kwa sasa anamalizia shahada yake ya Uzamivu katika Imani, Kazi na Uchumi katika Seminari ya Asbury Jimbo la Kentucky nchini Marekani.

Kwa Johnson, kila kitu ni kitakatifu katika Bwana. Na huu ndio mtazamo ambao ulimwezesha kuanzisha huduma ya Markaz Al Bishara, ambayo maana yake ni ‘Kituo cha Habari Njema’. Kupitia miradi 28 iliyokusudiwa kueneza Injili na mingine kuanzilishwe, huduma hii kwa kweli ni mfano bora zaidi wa kuendesha kazi ya biashara na umisheni kuwa pamoja.

Kituo cha Markaz Al Bishara hutoa huduma za kambi za watoto, huchimba visima vya maji, huhubiri Injili kwa njia ya redio, na hutoa mikopo midogo midogo kwa watu ili kuanzisha biashara zao. Pia kituo kimejitosa katika huduma za kusaidia watu waliopatikana na majanga mbalimbali na hujenga nyumba za bei naf uu kwa jamii za vijijini. Nyumba zaidi ya 220 za bei nafuu tayari zimeshajengwa. Yeye akiwa msomi, Asare ameanzisha Chuo cha Afrika kinachotoa mafunzo mara mbili kwa mwaka kwa waanzilishi wa makanisa na wafanyakazi kutoka nchi 30 za Afrika.

Markaz Al Bishara ina idara kubwa ya kusimamia kituo cha malazi na mikutano cha Radach chenye uwezo wa kuchukua watu zaidi ya 500,000 kila mwaka kwa mikutano mbalimbali. Zaidi ya asilimia 90 ya wageni wanaotumia Kituo hiki huwa siyo wa imani ya kikristo. Kituo cha malazi na mikutano cha Radach ni rasilimali ambayo inategemeza shughuli za huduma kifedha kwa asilimia 90.

Akiwa amefanya kazi sambamba na SIM kwa miaka 30, Johnson ni kijito kinachobubujisha hekima na kicheko. “Nimefanya makosa mengi, na makosa hayo yamenipa uzoefu mwingi. Mungu ametumia makosa yangu kufanya vitu vingi,” anasema Johnson.

Miaka 25 iliyopita, Johnson alishirikisha wazo la kuanzisha mradi ambao ungesaidia kuzalisha pesa za kuendesha umisheni. Wakati huo, wazo hilo halikuonekana kama ni wazo lenye manufaa kwa huduma. Kwa hiyo, alijitolea yeye mwenyewe kulifanyia kazi wazo hilo. Alianzisha biashara ndogo ndogo ili kupata mtaji kwa mtaji kwa mradi mkubwa; akaanza kununua na kuuza mchele, njugu na nafaka zingine.

Pia Wakristo wengi wenyeji walisaidia kupata asilimia 75 ya pesa za kuanza mradi ambao ungeweza kutegemeza kazi ya Injili. Kati ya dola milioni 2 zilizokuwa zinahitajika, Johnson aliweza kukusanya dola 500,000 kama msaada kutoka nje; na dola milioni 1.5 zilikusanywa kutoka ndani ya nchi.

Mafunzo kutoka Msamaria Mwema

Wakati Johnson alipokuwa anasikia kwa nguvu msukumo wa ndani wa kufanya biashara kwa kusudi la kusaidia kueneza injili, mfano wa Msamaria Mwema ulizungumza naye kwa sauti kubwa kutoka ndani ya moyo wake. Kutokana na mfano huu, Johnson alipata tabia/sifa nne za Msamaria Mwema zilizomfanya awe mfano kamili katika kuelezea upendo.

  1. Huruma: Msamaria Mwema alikuwa na huruma. Miongoni mwa watu wote waliopita alipokuwa yule mtu aliyekuwa amepigwa na wanyang’anyi na kuachwa akiwa mahututi, ni Msamaria Mwema pekee ndiye aliyekuwa na huruma ya kumsaidia.
  2. Uwezo wa kutenda: Msamaria Mwema alikuwa na uwezo wa kufanikisha mambo yake. Aliweza kumpa huduma ya kwanza kwa kumsafisha na kumfunga vidonda na kuifanya hali yake iwe imara kiasi cha kuendelea na safari mpaka alipomfikisha kwenye nyumba ya wageni.
  3. Uwezo wa kiuchumi: Msamaria Mwema alikuwa na fedha za kumlipa mtunza nyumba ya wageni, na kuahidi kuwa angekuja kulipa madeni yote ambayo yangesalia katika kumhudumia yule mjeruhiwa.
  4. Ujasiri: Msamaria Mwema alikuwa jasiri kiasi cha kusimama na kumsaidia Myahudi. Tendo hilo ni ajabu kwa maana Wasamaria na Wayahudi huwa wanachukiana.

Kati ya tabia/sifa hizi nne, Johnson aliona wamishonari wengi wanapungukiwa na sifa ya tatu – uwezo wa kiuchumi. Na Johnson alitafuta kuondoa upungufu huu kwa kutumia kila alichokuwa nacho. Ulemavu huu wa kiuchumi ndio ambao umefanya mashirika mengi ya kimisheni kutegemea sana msaada kutoka nchi za nje. Matokeo yake, mashirika mengi yamekufa kwa haraka sana. Johnson alihitaji kufanya jambo la asili na ambalo lingetokana na mazingira ya nyumbani na ambalo lingekuwa endelevu.

“Afrika inaweza kufanya kile kinachofanywa na nchi za Magharibi. Tumetegemea nchi za Magharibi kwa muda mrefu; tunahitaji kuhifadhi utu wetu” anasema Johnson.

Ukilinganisha kuenea kwa Ukristo na Uislamu katika nchi ya Ghana ndiko kulimfungua macho Johnson. Anaelezea jinsi walimu wa Kiislamu walivyokuja Ghana kama wafanyabiashara miaka 450 iliyopita. Walifanya biashara ya kola, pilipili, chumvi na dhahabu kwenye ukanda wa Volta. Walitajirika na mwishowe wakawa washauri wa machifu.

Wakristo, kwa upande mwingine, walifika sehemu ya kusini mwa Ghana wakiwa na pesa kutoka Magharibi, mwisho wake wakasababisha utegemezi. Zaidi ya asilimia 95 ya mashirika yaliyotegemea ufadhili kutoka ng’ambo yalikufa. ‘Zalisha pesa zako mwenyewe na pesa hizo zitaongezeka’, anashauri Johnson. ‘Maendeleo ni polepole; nenda hatua kwa hatua, na Mungu atakubariki’.

Upendo wa Mungu unaweza kuenezwa kwa njia nyingi, mara nyingi bila maneno. Ikiwa na wafanyakazi 168, na wafanyakazi wa kujitolea zaidi ya 300 huko Tamale, katika moja ya majimbo maskini zaidi ya nchini Ghana, huduma inaeneza upendo wa Kristo kama moto wa mwituni wa Australia.

Kwa Johnson, kazi ni kitendo cha ibada. “Mimi ni mkulima, mchungaji, mfanyabiashara, na mwandishi.

Mungu ndiye sababu ya kila kitu ninachofanya. Hakuna kazi takatifu na hakuna kazi ya kidunia. Kila kitu ni kitakatifu kwa Bwana. Biashara ni tendo la ibada,’’ anasema Johnson. Tusitenganishe imani na biashara. Tunatakiwa kuviweka vyote pamoja na kutafuta njia za kuzifanya zikamilishane.

“Mungu hakuumba meza’’, anasema Johnson. “Mungu aliumba miti. Mungu anataka sisi tutumie bongo zetu.”

Mchungaji Johnson Asare ni mkurugenzi wa kituo cha mikutano cha Radach, Tamale,Ghana (www.radach.org). Ni mwanzilishi na mkurugenzi wa kitaifa wa huduma za Markaz Al Bishara (www. bisharapraise.radach.org) . Ameandika vitabu na ni mnenaji wa masuala ya Biashara ya Kimisheni. Unaweza kuwasilina naya kwa: Johnson@radach.org

Biashara ya kimisheni ni nini?

Biashara za Kimisheni (BK) ni kazi za kibiashara za wakristo wakiwa na nia ya kutumia biashara hizo kufanya kazi za misheni. Wamishonari wanaojihusisha na biashara za kimisheni wameitwa na Mungu na kutumwa na kanisa kushirikisha watu wengi injili ya Kristo na kuwafanya watu kuwa wanafunzi katika tamaduni zote, wakitumia stadi zao za biashara. Makundi ya aina kadhaa za BK yana msisitizo tofauti tofauti, lakini yote yanatumika kwa ajili ya kazi za umisheni.

1.Biashara kama Umisheni

“Business as Mission” (BAM) inahusiana na biashara inayotumika kama ukumbi halisi wa huduma. Hawa wahudumu wa kimisheni wanatumia mawasiliano kupitia michakato ya kawaida ya kufanya biashara, kama vile waajiriwa, wasambazaji wa vifaa, wateja, wafanyakazi wa serikali na washirika wa biashara. Biashara hii hufuata mifano ya kanuni za kibibilia na huleta amani (shalom) kwa jamii ya wenyeji.

2.Biashara kwa ajili ya Mabadiliko

“Business for Transformation” (B4T) ni aina ya biashara ambazo zimewekwa kimkakati katika maeneo ambapo Kristo hajulikani au anajulikana kwa kiasi kidogo. Zimeundwa kubuni ajira, nia ikiwa ni kuleta mabadiliko katika sehemu ya jamii, na hasa kupitia uinjilisti, ufuasi na uanzilishi wa makanisa.

  1. Biashara yenye malengo ya Umisheni

“Business- based mission” (BBM) inamaanisha aina ya biashara inayotumika kama njia kwa wamishonari kufanya kazi ya umisheni katika nchi. Pale ambapo biashara inafanikiwa, inaweza kulipa sehemu au mishahara yote ya mishonari. Kimsingi kusudi la huduma ni nje ya biashara, ingawa baadhi ya huduma zinaweza pia kuchanganya biashara na huduma. Kazi ya kutengeneza mahema kama ile iliyokuwa inafanywa na Mtume Paulo ni moja ya ina za BBM.

  1. Biashara kwa ajili ya umisheni

“Business for Mission” (BFM) ni miradi yenye kusudi la msingi la kutengeneza faida ili kusaidia kazi za misheni. Kama BFM, matumizi ya faida inayotarajiwa lazima ielezwe na kutengwa kwa ajili hiyo katika mwanzo wa kuanza shughuli za biashara husika. Mifano inaweza kuwa kama vile kuwa na Kampuni ya kusafirisha watalii ambayo inaweza kuwa inatoa tiketi maalum kwa ajili ya wamishonari au kuwa na kampuni ya uchapishaji ambayo ni maalum kwa ajili ya kuchapisha nakala kwa matumizi ya kazi za misheni.

  1. Taasisi ndogo za Fedha

Taasisi ndogo za kifedha hutoa mikopo midogo kwa mtu mmoja binafsi au kwa makundi ili kuwasaidia kuanza biashara ndogo ndogo. Taasisi hizi zinafaa sana kwa jamii maskini zaidi, mahali ambapo fursa za ajira ni haba. Shirika linalotoa mitaji pia hutoa mafunzo kwa wapokeaji wa mikopo na husimamia utaratibu mzima wa mikopo. Maneno kama taasisi za kukopesha, biashara ndogo ndogo au ujasirimali mara nyingi hutumika kumaanisha taasisi zinazotoa mikopo midogo midogo.

share
share
Instagram
contact us
contact us
contact us