Maono ya Mungu yanakutana na ufadhili wa Mungu
Kate Azumah
Ili kuunganisha nchi baada ya vita vya wenyewe kwa wenyewe vya Nigeria, mkuu wa jeshi wa wakati huo, Jenerali Yakubu Gowon, alianzisha programu mnamo 1973, kupeleka wahitimu wa taasisi za elimu ya juu kuhudumu kote nchini. Miongoni mwa waliotumwa Jimbo la Kaduna mnamo 1974 walikuwa viongozi wa Kikristo wa chuo kikuu. Kinyume na uzoefu wao kusini, waliona uchache wa makanisa na shughuli za uinjilisti kaskazini, na hii iliwatia msukumo wa kuandaa huduma ya Filamu ya Yesu katika jiji la Zaria mnamo Desemba mwaka huo.
Wakazi wa eneo hilo walikuja kwa wingi na kuitikia mwito wa kuokoka uliofuata. Hata hivyo, baadhi ya Waislamu walishambulia baadaye, na kuharibu vifaa na kuwapiga kwa mawe wanachama wa kikosi cha vijana. Wengi waliishia hospitalini, na wote walishangazwa na tukio hilo.
Wakati waandaaji walipokusanyika tena mwaka uliofuata, Bwana aliwapa maono ya kuendelea na kuhubiri injili kwa Waislamu na wale walio katika nchi za Afrika Magharibi zinazoongea Kifaransa. Hivyo basi, CAPRO (Calvary Productions, sasa Calvary Ministries) ilizaliwa—shirika la kimishenari la wazawa lenye wamisionari 800 katika nchi 44, na shule za mafunzo ya umisheni nchini Nigeria, Cote d’Ivoire, Kenya, India, Marekani, Uingereza, na Sudan. Je, wamefadhili vipi haya yote? Mkurugenzi wa kimataifa wa CAPRO, Dondo Iorlamen, anatueleza zaidi.
Jukumu la wote
“Waanzilishi wetu walitiwa moyo na imani ya wamishenari wa Magharibi ambao waliamini kwamba maombi pekee ndiyo yalihitajika na Mungu angewapa kinachohitajika. Baada ya muda, walijifunza kwamba umisheni ulikuwa ni wajibu wa Kanisa zima na wakarekebisha mbinu zao. Mbali na maombi, walikaribisha msaada kutoka kwenye Mwili wa Kristo kwa kushirikisha taarifa na mahitaji ya kuombea.”
Mikono “inayotuma” na “in ayokwenda”
CAPRO hupanga programu mbili kwa ajili ya mtu yeyote ili aweze kushiriki katika umisheni. Ya kwanza ni Programu ya Uanafunzi na Kuufahamu umisheni (D-MEP). Hii hudumu kwa wiki 12 katika shule, vyuo vikuu, makanisa, taasisi za kitheolojia, na mashirika mengine ya kitaaluma. Ya pili ni tukio la kila mwaka linaloitwa “Kusanyiko la Siku za Mwisho.”
Wamisionari wa CAPRO katika mkutano
Waamini wanaoshiriki katika programu wanaonyeshwa takwimu za kimisheni, makundi ya watu ambao hawajafikiwa, na wajibu wao wa kushirikisha injili. Wanaalikwa kufanya maombezi, kutoa pesa kwa ajili ya umisheni, au kwenda shambani kama wamishenari.
Wanaoitikia hupangwa katika mfumo wa usaidizi unaoitwa sura ya CAPRO. Wale wanaojiandikisha kuwa wamishenari wanakuwa wafanyakazi wa ofisi au wamishenari wa shambani na kwa pamoja wanaunda mkono wa CAPRO “unaoenda”. Wale waliosalia katika sura kwa ajili ya kusaidia ni mkono “unaotuma”.
Kuifadhili kazi
Wamishenari wa CAPRO hupitia mwaka mmoja wa mafunzo ya umisheni na wanahojiwa ili kubaini kama ni watu sahihi kwa ajili ya CAPRO. Dondo anaeleza, “Mtu anaweza kuwa mzuri, lakini asiitwe kufanya kazi na CAPRO. Tunawaambia wamishenari wetu kwamba hawatapokea mishahara yoyote kutoka kwenye huduma— nikiwemo na mimi mkurugenzi wa kimataifa. Mishahara ingekuja tu kupitia kwa Bwana na watu wake. Tunaamini kwamba Mungu akimwita mtu yeyote, atampatia mahitaji yake.”
“Jambo la kwanza kuhusu kufadhili umisheni ni kuhakikisha kwamba unachotaka kufanya ni mpango wa Mungu. Ikiwa ndivyo, Bwana atalifadhili. Kazi ya mmishenari ni kuomba na kugundua kile Bwana anataka kufanya. Ikiwa Bwana hatatoa, pengine sio mradi wake au sio wakati wake.”
“Kinachofuata, chochote ambacho Bwana anaweka moyoni mwako kufanya, kiandike na uongeze bajeti. Wamishenari wetu huwasilisha mipango yao iliyoandikwa ili kuidhinishwa, na kwa pamoja, tunaomba na kumwamini Mungu kufadhili kadili  wamishenari wanavyoshirikisha familia, marafiki, na washirika wa kanisa. Tunawatia moyo wamishenari wetu kutoa kwa ajili ya mradi kwanza, kwa sababu kiroho, hii itavutia watu wengine kutoa pia. Tuna kiwango cha chini wanachopaswa kupata kabla ya  kuondoka kwenda shambani. Inapohitajika, ofisi huingilia kati kutafuta wafadhili kwa ajili ya wamishenari wanaotatizika.”
“Hapo awali, tulijaribu baadhi ya shughuli za kujiongezea kipato, lakini zote zilishindikana. Tulitambua kwamba Mungu hakutaka tujihusishe na shughuli zozote za kibiashara ili kufadhili kazi yake. Hata hivyo, watu binafsi katika huduma wanaweza kujihusisha na biashara mradi tu haiingiliani na wito wao. Wakati mwingine, biashara kama hizo hufungua milango kwa mwingiliano mzuri kwa ajili ya injili.

Ofisi ya kimataifa ya CAPRO
Mwanzo mgumu
Safari ya CAPRO ya takriban miaka 50 imekuwa ngumu katika baadhi ya maeneo, ikiwa ni pamoja na mizozo ya uongozi, wamishenari wasioridhika, Kanisa la Nigeria ambalo halikuelewa umisheni wakati huo, na baadhi ya wamishenari wa Magharibi ambao hawakukubali Waafrika kama wenzao halisi.
“Shirika moja la kimisheni ambalo liliambatana pamoja nasi katika nyakati hizo ni WEC (Uinjilishaji wa Ulimwengu wote kwa ajili Kristo). Pamoja na msaada wa Mungu, waliipa CAPRO mafunzo na uzoefu. Wakati viongozi wetu walipokabiliwa na ukosoaji na kukatishwa tamaa, WEC iliitia nguvu mikono yao.
Dondo anasimulia kwamba akiwa mmishenari kijana wa CAPRO mwenyewe miaka ya nyuma, alilazimika kumlisha mke wake kwa panzi na majani, lakini leo, hakuna mmishenari wa CAPRO anayelala njaa. Huenda wasile wanachopendelea, lakini chakula si tatizo. Mungu anafanya mambo makubwa zaidi.
Uaminifu wa Mungu
“Wamishenari wetu walikuwa na wasiwasi kuhusu ufadhili wa elimu za watoto wao, lakini Mungu amemchagua mtu wa kushughulikia hilo. Sasa, kila mtoto wa mmishenari wa CAPRO anayeingia katika taasisi ya elimu ya juu anapata ufadhili kamili. Takriban watoto wa wamishenari 200 wanafaidika kwa sasa.
“Wamishonari wetu wanalipa kodi za nyumba ulimwenguni kote, baadhi yao ni Paundi 400 za Uingereza na Paundi 800 kila mwezi. Je, wanafanyaje? Bwana hutoa. Wakati wa vita vya Sudan, ilitubidi kuwahamisha na kuwapa makazi mapya wamishonari 17. Walikaa kwa miezi miwili barabarani, lakini Mungu alituandalia kiasi kikubwa tulichohitaji katika hali hii ya dharura.”
“Ofisi yetu ya kimataifa ilikuwa ya kukodi, lakini tuliinunua ndani ya siku 90 mwenye nyumba alipotaka kutuuzia. Haya yote ni uaminifu wa Mungu katika kutufadhili; hatukuwahi kukopa kufanya lolote kati ya hayo. Lakini ushuhuda mkuu zaidi ni kuona makundi ya watu ambao hawajafikiwa hapo awali yakimjua Yesu Kristo kama Bwana na Mwokozi.”
Umisheni wa Africa
Dondo anasema kuwa takriban asilimia 80 ya wafadhili wa CAPRO ni Wanaijeria, lakini wanatumai watu wengi zaidi katika nchi nyingine watashiriki katika ufadhili huo. Wengi wa CAPRO ni Waafrika pamoja na Waasia na Waamerika wachache. Makanisa 344 yaliyopandwa na CAPRO hayana ulazima wa kutuma msaada wowote kwa ofisi ya CAPRO; badala yake, yanatiwa moyo kutuma wamishenari wao wenyewe.
Afrika imekuwa kitovu kipya cha mvuto cha Ukristo wa ulimwengu, na ikiwa Bwana anatuita tuendeleze utume wake kwa maeneo ambayo hayajafikiwa, basi amefanya rasilimali zote zipatikane—kupitia watoaji wake watiifu na kwa moyo mkunjufu katika Kanisa lake la Kiafrika lililojaaliwa vema.
TAFADHALI OMBA
- Mshukuru Mungu kwa uaminifu wake kwa wamishenari wa CAPRO kwa miaka mingi.
- Ombea wamishenari wote wa Kiafrika kupokea kila msaada wanaouhitaji.
- Ombea mawazo bunifu ya ufadhili kwa mashirika ya kimisheni ya Kiafrika.