“Nilianza kwa kuwa Mwislamu” – nyakati za wamishenari
John, mmishenari nchini KenyaBaba yangu alikuwa Mkatoliki, na alikuwa akisoma Biblia huku akiandika maelezo kwenye daftari. Nilianza kusoma Biblia ili kumfurahisha, lakini sikuhisi mguso ule uliomfanya alie kila alipokuwa akisoma. Baba yangu alipofariki, ndugu zangu wote walisilimu. Dada yangu mkubwa ndiye pekee alibaki Mkristo.
Maisha yalikuwa magumu kwa sababu sikuwa Mwislamu — nilijihisi mpweke sana hasa katika nyakati kama Ramadhani. Hivyo, nami nikawa Mwislamu. Dada yangu aliposikia kuwa nimekuwa Mwislamu pia, alihuzunika sana. Akanisihi nisome vitabu vya Yohana, Matendo ya Mitume, na Warumi. Nilifanya hivyo ili kumfurahisha, lakini jambo la ajabu lilitokea — yale niliyokuwa nasoma yalikuwa tofauti sana na yale tuliyofundishwa katika Uislamu. Nilihisi kile baba yangu alikuwa akihisi; nilikuwa nasoma huku nikilia.
Nilitamani kusoma theolojia ili nirudi na kuwahubiria ndugu zangu. Lakini kwa kuwa walikuwa Waislamu, hawakuwa tayari kugharamia masomo hayo. Badala yake nikasomea ufundi (mekanika), jambo ambalo halikuwa matakwa yangu.
Siku moja, mtu kutoka Kenya alikuja kanisani kwetu kuzungumzia huduma ya umishenari. Aliniongoza kwenda katika moja ya shule za umishenari nchini Kenya. Nilisoma kwa mwaka mmoja, na leo mimi pamoja na mke wangu ni wamishenari wa kwanza miongoni mwa kundi la watu ambao hawajafikiwa katika sehemu za Kusini na Pwani ya Kenya.